Showing posts with label Siasa. Show all posts
Showing posts with label Siasa. Show all posts

NIMRODI MKONO naye apinga serikali tatu, adai kuwa, una lengo la kutugawa kama kipindi cha ukoloni

Mjadala unaoendelea kuhusu rasimu ya Katiba Mpya, unayagusa makundi mengi ya kijamii na watu binafsi, kila upande kwa namna yake.
Lakini sehemu kubwa ya mjadala huo imejikita katika muundo wa utawala wa nchi, ambapo rasimu hiyo iliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Katiba, imependekeza kuwapo serikali tatu. Pendekezo hilo, limechukua sehemu kubwa katika mjadala unaoihusu rasimu hiyo.
Mmoja wa watu ni Nimrodi Mkono, Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM) na mwanasheria aliyebobea katika tasnia hiyo kwa miongo kadhaa sasa.
Mkono, anajenga hoja yake juu ya msingi kwamba, Katiba inafaa kuwapo, lakini haipaswi kuwa jambo lenye uzito kiasi cha ‘kuteka’ mapokeo na nia chanya za viongozi waasisi katika nchi za Afrika, hususani kuhusu umoja wa nchi hizo na kupunguza wingi wa serikali zenye mamlaka kamili.
Ndiyo maana, Mkono anasema mfumo wa serikali tatu katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, utakuwa muendelezo wa mbinu za kikoloni, wenye lengo la kuwagawa wananchi na kutoa fursa pana ya uporaji wa rasilimali za nchi.
Hivyo anasema, kiongozi yeyote anayeutetea mfumo huo, hapaswi kuutumikia umma wa Tanzania, hasa katika nafasi ya Urais.
Kwa mujibu wa Mkono, Katiba si kitu kinachohitaji nguvu kubwa, badala yake nchi inaweza kuweka mambo ya msingi yan
ayopaswa kukubalikuwa, kufuatwa na kutekelezwa kama ilivyo kwa Uingereza.
“Wanaotaka serikali tatu, binafsi ninawaona kama wenye fikra mgando, hawayaishi mambo mema yaliyoasisiwa na viongozi katika nadharia ya kuwapo Afrika moja, tukagawanywa na wakoloni na sasa wanataka kuigawa Tanzania,” anasema.
Mkono anasema tangu wakati wa ukoloni, Waafrika walikuwa wamoja, wakitendewa uovu na wakoloni walioingia barani humo kwa lengo la kupora rasilimali zao.
“Sasa wanaotaka Tanzania igawanyike na kuwa na serikali tatu, wanafanya hivyo kutoa mianya ya wazungu kuendelea kupora rasilimali zetu, watu wa aina hiyo hawafai kuwa marais wa nchi hii,” alisema.
Mkono anasema hoja hiyo alitaka kuiwasilisha bungeni mjini Dodoma, lakini ikadhibitiwa kwa mujibu wa kanuni zinazotoa muda mfupi kwa Mbunge kuzungumza.
Hata hivyo, Mkono, anasema ili Tanzania ijiimarishe kwa umoja, amani, utulivu, maendeleo na ustawi wa jamii, inahitaji kubaki katika mfumo wa serikali moja na kuwa na kiongozi mkuu (Rais) anayesimamia maslahi ya umma pasipo mgawanyiko.
AWASHANGAA WARIOBA, SALIM
Mkono anasema, inashangaza kuona wajumbe wa Tume ya Marekebisho inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, kuwasilisha pendekezo la serikali tatu, huku wakiwa na uelewa wa kihistoria kuhusu umoja wa kuwapo umoja barani Afrika.
Ingawa hakuwataja kwa majina, Mkono, akaisema wapo watu waliowahi kuwa katika kundi G55 lililoibua hoja ya kuwapo serikali ya Tanganyika, na sasa wanataka kuifanikisha azma hiyo kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jaji Warioba, anatajwa kuwa miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walioibua hoja ya Utanganyika mwaka 1994, wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, ambayo hata hivyo, ilizimwa kwa msaada wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Mkono, anasema pia kuwa katika tume ya Warioba, yumo mjumbe aliyewahi kuwa kiongozi wa juu katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), aliyetekeleza jukumu ya kuihubiri ‘Afrika moja’, lakini sasa ameingia katika orodha ya wanaotaka kuigawa Tanzania.
Mjumbe wa tume hiyo, Dk. Salim Ahmed Salim, alikuwa Katibu Mkuu wa sita wa OAU, ambaye kumbukumbu zinaonyesha aliifanya kazi hiyo kati ya Septemba 19, 1989 hadi Septemba 17, 2001.

From: nipashe jpili

Mbunge kigwangala asema ""SIWEZI KUMPIGIA KURA LOWASA KAMWE ENDAPO ATAGOMBEA URAIS, ATOA SABABU"




Mbunge wa Nzega Hamis Kigwangalla amesema hawezi kumpa kura yake Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli Mheshimiwa Edward Lowassa endapo jina lake litajitokeza kama mmoja ya wagombea urais, ni kauli ya Kigwangalla akijibu swali aliloulizwa na Mtangazaji Fina Mango katika kipindi cha Makutano kuhusu vuguvugu la urais 2015 linaloendelea ndani ya CCM juu ya mgombea urais ambapo Edward Lowassa ni kati ya wanaotajwa sana kama wagombea hasa katika mitandao ya kijamii.
“Sitompa kura Mheshimiwa Edward Lowassa kwa sababu za msingi tu, kwamba ninakipenda chama changu na nina hakika chama changu kikija na mgombea kwenye uchaguzi mkuu 2015 ambaye ana historia ya kuhusishwa na mambo machafu kama yale ya Richmond, Dowans ambayo unayasema, hapa tunaweza kupata tabu sana kuomba kura kwa wananchi, lakini p
ia tutakuwa tumewapa hoja wapinzani wetu ya kusema tunalea ufisadi, tunaubembeleza ufisadi kwa mikono miwili’ Kigwangalla
Kwenye sentensi nyingine Kigwangalla amesema Tanzania aihitaji rais asiyeweza kusimamia ukweli ambapo kuhusu ishu ya dowans amesema haoni tatizo la mitambo hiyo isipokuwa uamuzi uliotumika katika upatikanaji wake.
Kwenye hii interview, Kigwangalla alitangaza nia ya kugombea urais mwaka 2025 na kusema 2015 anaona bado ni mapema kwake kwani anaamini watanzania bado hawajamjua Hamis Kigwangalla ni mtu wa aina gani.

IDDI AZAN (Mbunge wa Kinondoni) ajibu uvumi uliosambaa kuwa anajihusisha na MADAWA YA KULEVYA





Yafuatayo ni maneno maswali na majibu aliyoyatoa kwenye interview na Mussa Hussein wa Jahazi Clouds FM.
d Azan ambae ni mbunge wa jimbo la Kinondoni ameongea kuhusu tuhuma nzito zilizosambaa kwenye mitandao baada ya kutajwa kwenye barua ya Mtanzania anaedai kufungwa gerezani Hongkong kwamba ni mmoja wa matajiri kwenye biashara ya dawa za kulevya Tanzania.
Vipi kuhusu hizi tuhuma Mheshimiwa?
“Hata mimi mwenyewe sijui tuhuma hizi wapi zimeanzia, ila nakumbuka mwaka  jana kuna baadhi ya viongozi wa CCM walisema kwenye mkutano wa vijana kwamba mimi najihusisha na biashara hii haramu. Nikachukua hatua ya kuwaatarifu polisi na waliwahoji wale watu kilichoendelea wanajua wao polisi kwasababu mimi niliwaachia wao. Lakini hivi sasa hili swala limejitokeza tena kwa namna nyingine. Kuna mfungwa ambaye sijui yupo China au Hongkong ameandika barua na ipo kwenye mtandao na watu wameshaanza kunihukumu. Kitu cha kwanza naweza kusema kwamba hii barua ni ya uongo, mimi sijihusishi na biashara ya madawa ya kulevya na wala sijawahi kujihusisha na biashara yoyote haramu. Kingine mfungwa mwenyewe hakusema yeye ni mfungwa namba ngapi au kafungwa gereza gani ili tuweze kumfuatilia atoe ushahidi zaidi. Hiki kitu mimi nimekichukulia hatua za kisheria, nimeitaarifu polisi juu ya hili swala tena. Hii ni mara ya pili nataka haki itendeke, mimi siko juu ya sheria natakiwa nifate sheria kama nahusika na hiyo biashara hatua zichukuliwe.”
Lakini kwanini ni wewe tu mara ya pili hii na sio waheshimiwa wengine?
“Hata sijui kwa nini mimi tu,chanzo nadhani kilianza kwanini anatembelea magari mazuri . Wakaanza kuuliza anafanya biashara gani huyu au anaunza unga au hivi na vile ndiyo ikawa hivyo.Labda jinsi ninavyojihusisha na wananchi wangu kwa karibu najichanganya pamoja nao labda hilo linawafanya waweze kuongea hivyo. Kingine jinsi ninavyokubalika kwenye jimbo langu, ukifuatilia kwa makini tuhuma iliyopita ilitoka wakati tunaelekea kwenye uchaguzi na hivi sasa tupo kwenye safari ya kuelekea kwenye uchanguzi tayari maneno kama haya yashaanza kutoka. Sasa kuna watu wananiogopa kwenye jukwaa kwamba nikisimama nao hawaniwezi kabisa sasa wanajaribu kunichafua ili kuniondoa kwa kuwambia wananchi kuwa mimi sifai. Huu ni ugomvi wa kisiasa sana.”
Mheshimiwa kama huu ugomvi ni wa kisiasa unadhani utakuwa unatoka ndani ya chama cha CCM au nje?
“Mimi naamini ni ndani ya CCM kwasababu waliotamka maneno haya hapo zamani ni viongozi wa CCM wakubwa tu tena ngazi ya mkoa pia hata kabla ya mwaka 201o kwenye uchaguzi wa kura za maoni kuna viongozi wa CCM pia walizungumza maneno haya.”
Vipi kuhusu wananchi wa Kinondoni ambao ndiyo wapiga kura wako ambao wamekutana na hali ya sintofahamu, nia bado ipo kwa mwaka 2015?
“Naomba niwaondoe wasiwasi wananchi wa Kinondoni, mimi nitaendelea kuwa mwadilifu kwenye kazi, siwezi kukiuka maadili ya kazi yangu. Kuhusu mimi mwaka 2015 ni mapema sana kuzungumzia. Lakini panapo majaaliwa ya kiafya basi tutagombea. Nikisema hivi najua watu hawa wanazidi kuumia kwasababu wanajua nikisisimama mimi jinsi nilivyokaribu na watu wangu lazima nitachukua kiti.”

HII KALI: Wanachama wa CHADEMA wapata dhamana, watoka gerezani, wasimulia walivyoteswa, waambiwa wawasingizie mbowe na slaa UGAIDI


HATIMAYE makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaokabiliwa na shtaka la kummwagia tindikali kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wameachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga.

Makada hao ambao wanatetewa na mawakili Prof. Abdallah Safari na Peter Kibatala ni pamoja na Avodius Justinian (Bukoba), Oscar Kaijage (Shinyanga), Rajabu Daniel (Dodoma), Seif Magesa (Mwanza) na Henry Kileo (Dar es Salaam).

Muda mfupi baada ya kuachiwa, vijana hao walifichua jinsi walivyopata mateso makali kutoka kwa maofisa wa jeshi la polisi wakilazimishwa kuwataja viongozi wa juu wa CHADEMA, Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, John Mnyika na Tundu Lissu kuwa wanahusika na ugaidi.

Bila kumung’unya maneno waliwataja vigogo kadhaa wa serikali, CCM na mbunge mmoja wa CHADEMA kuwa ndiyo waratibu wa mikakati hiyo ya kuwabambika CHADEMA kesi za ugaidi.

Vijana hao waliowasili mjini Igunga 12:45 jioni juzi na kupandishwa kizimbani katika mahakama hiyo saa 1:20 usiku na kusomewa shtaka lao la kufanya kitendo kilicholenga madhara mwilini.

Mapema hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Mrakibu Msaidizi, Cosmas Mboya, makada hao walidaiwa kutenda kosa la kummwagia tindikali kada wa CCM, Mussa Tesha, usiku wa Septemba 9, 2011, katika msitu wa Hanihani, Igunga.

Mbela ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ajali Milanzi, ilidaiwa na mwendesha mashtaka kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walimmwagia kada huyo tindikali sehemu za uso, puani, mdomoni na kwenye bega la kulia.
Mwendesha mashtaka alidai kuwa shauri hilo limekwenda wilayani Igunga baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, kuwafutia shtaka la ugaidi na kuamuru kwamba warejeshwe Igunga na kushtakiwa kwa kosa la kumwagia tindikali kisha wapatiwe dhamana.

“Masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama ni kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana kwa ahadi ya sh milioni 10 za maandishi kila mmoja.
Washtakiwa wote walikana shtaka hilo na kutimiza masharti ya dhamana kisha hakimu akaiahirisha kesi Septemba 10 mwaka huu itakapotajwa tena.
Katika hatua nyingine, vifijo, nderemo, vilio vya furaha na shangwe vilitawala mahakamani hapo baada ya makada hao kuachiwa kwa dhamana.
Wafuasi wa CHADEMA walifanya maandamano yaliyoongozwa na msururu wa magari, pikipiki na baiskeli wakitembea umbali wa takriban kilomita tano kutoka mjini Igunga kwa lengo la kuwapokea makada hao.
Akizungumza kwa kifupi, wakili wao Peter Kibatala, aliendelea kuishukuru Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa kuonyesha ujasiri wake na kutimiza majukumu yake ya kutoa haki.
“Namshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Simon Likelerwa, kwa weledi wake wa kutoa uamuzi ulio sahihi kisheria na ulioshiba.
“Pia naipongeza mahakama ya Igunga kwa kuwapatia dhamana washtakiwa kwa masharti yanayoendana na uzito wa jambo lenyewe kwani dhamana ni haki ya msingi kwa mshtakiwa yeyote,” alisema.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Tabora, Kansa Mbaruku, alisema kuwa pamoja na kuridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, pia hiyo ni ishara kuwa haki imezingatiwa kisheria.
Awali makada hao walifutiwa mashtaka na mahakama ya wilaya ya Igunga kisha kukamatwa tena na kupelekwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kusomewa shtaka la ugaidi ambalo hata hivyo lilifutwa na mahakama hiyo.

Mikakati ya hujuma 
Wakisimulia kile kilichowapata tangu kukamatwa kwao hadi kufikishwa mahakamani, makada hao walisema kuwa walipata mateso makubwa huku wakilaghaiwa kupewa vyeo serikalini na fedha ili mradi wawahusishe viongozi wa CHADEMA na ugaidi.

Evodius Justinian (Bukoba)
Alisema kuwa alikamatwa Bukoba: “Nikakaa rumande siku tatu kabla ya kusafisirishwa hadi Mwanza. Nikiwa huko niliteswa sana ili nikubali kuwa ninajua ule mkanda wa Wilfred Lwakatare uliokuwa kwenye mitandao.
“Nilikataa, niliteswa sana nikahojiwa kama nilimmwagia Musa Tesha tindikali nilikataa. Nilisafirishwa kwa ndege kuja Dar es Salaam ambako nilipokelewa na polisi.

“Nikiwa uwanja wa ndege niliomba ruhusa kwenda chooni, askari walinifuata huko wakanitesa sana. Nilifanyiwa mahojiano na Advocate Nyombi na afande Pasua. Walinilazimisha nikubali kuwa viongozi wetu huwa wanafanya vitendo vya kigaidi,” alisema.
Alisema kuwa akiwa makao makuu ya jeshi la polisi, aliteswa sana kwa maelekezo ya Afande Pasua na Nyombi katika ghorofa ya nane, jengo la makao makuu ya polisi.

“Niliambiwa nieleze siri za Dk. Slaa, Mbowe, Mnyika na Lissu na niseme kuwa walihusika na vitendo vya utekaji na utesaji, nilipokataa nilipigwa shoti za umeme ili nikubali kusema.

“Walikuwa wametafuta hata waandishi wa habari wakisubiri nikubali ili wanirekodi. Nilitoa maelezo kwa kulazimishwa huku nikiteswa. Nilipata nafuu baada ya wakili wangu, Nyaronyo Kicheere, kuja ndipo nikaeleza nilivyofanyiwa ukatili,” alisema.

Alisema kuwa alisafirishwa toka Dar es Salaam hadi Igunga na kwamba kila walipopita alitambulishwa kwa makamanda wa polisi kuwa ni mtu hatari sana.

Seif Magesa (Mwanza)
Alisema kuwa alikamatwa Mwanza na mabaunsa wa Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, aliyefukuzwa CHADEMA, wakiambatana na Adam Chagulani ambaye pia alifukuzwa pamoja na baadhi ya maafisa wa Usalama wa Taifa.

“Nilipelekwa ofisi za Usalama wa Taifa. Nilihojiwa nikiulizwa mimi ni nani katika CHADEMA na kwa nini huwa nawasiliana na Mbowe, Dk. Slaa, Lissu au Mnyika,” alisema.

Alisema kuwa aliuzwa kama viongozi hao wanahusika na utekaji wa watu mbalimbali unaotokea nchini na alipokataa aliteswa sana kuanzia saa 3 hadi 7 usiku.

“Nilipigwa shoti za umeme kwa maelekezo ya afande Pasua. Yeye alikuwa anakuja kuniaga kuwa anaenda kunywa pombe, vijana watafanya kazi yao. Waliniambia kuwa Lwakatare alikuwa amenitaja kuwa mimi nafanya vitendo vya kigaidi. Nilikataa kata kata,” alisema.

Aliongeza kuwa Aprili 23, mwaka huu, waliwaleta mama yake mzazi, mama mkwe na mkewe huku wakimdhalilisha mbele yao lakini alikataa kubadili maelezo yake.

“Siku moja nikiwa nahojiwa simu ya afande aliyekuwa ananihoji ilikuwa karibu; kiongozi mmoja wa CCM (anamtaja) alipiga simu akisema kama nimekataa kusema lolote nipelekwe Igunga ambako nilipelekwa nikasomewa shtaka la kummwagia tindikali Musa Tesha,” alisema.

Oscar Kaijage (Shinyanga)
“Mimi nilikamatwa, nikaambiwa niwasaidie askari kufahamu wizi wa milioni 100 uliokuwa umefanyika kwa njia ya mtandao kwa kuwa mimi ni wakala wa Airtel.

“Lakini nilipokubali kwenda na askari kituoni nikawekwa chini ya ulinzi. Ghafla nikapelekwa kwa mkuu wa upelelezi akanielekeza kuwa nikapekuliwe nyumbani kwangu kama kuna silaha ya aina yoyote au chupa zenye majimaji. Nilipekuliwa hawakupata kitu. Ilikuwa yapata saa 5 mchana,” alisema.

Aliongeza kuwa ilipofika saa 12 jioni, alipelekwa tena kwenye ofisi ya mkuu wa upelelezi, akakutana na askari alioambiwa wanatoka Dar es Salaam.

“Hapo nikamkuta afande ninayemfahamu, anaitwa Pasua kwa kuwa aliwahi kufanya kazi Shinyanga na Simiyu. Walinihoji kwa nini nina namba za viongozi wa CHADEMA. Nikawaabia, ‘mbona hamuulizi za wale wa CCM?’,” alisema.
Alisema kuwa alijibiwa kuwa wanajua hana kosa ila wanataka ushirikiano aseme kuwa Mbowe, Slaa, Mnyika na Lissu wanahusika na utekaji unaotokea nchini.

“Nilikataa. Afande Pasua nikamwambia anajua kazi yangu na mimi namjua yeye ndipo wakasema sasa kwa kuwa sitoi ushirikiano nitaunganishwa kwenye kesi ya kummwagia Musa Tesha tindikali huko Igunga,” alisema.
Aliongeza kuwa alipelekwa Igunga na wakati wanahojiwa na askari wa kutoka makao makuu, walikuwa wanafanya siri hata OCD wa pale alikuwa haruhusiwi kusikia.

Rajabu Kihawa (Dodoma)
Alidai kuwa alichukuliwa Dodoma baada ya kupigiwa simu na msichana mmoja aliyedai kuwa na maagizo kutoka kwa kaka yake anayesoma naye Chuo Kikuu cha Dodoma.

“Nilikataa lakini alikuwa anapiga simu kila mara, nikaona ngoja nikamsikilize. Nilipofika kabla sijaongea naye nilikamatwa na maafisa sita wa polisi waliojitambulisha, wakaninyang’anya simu zote na kunipeleka polisi.
“Walinihoji kama najua mkanda wa Lwakatare, nikasema sijui. wakanihoji kama viongozi wa CHADEMA wanahusika na utekaji unaoendelea nchini, nako nikasema sijui,” alisema.

Alisema kuwa baada ya hapo alipelekwa na kufungiwa Chamwino siku mbili bila kupewa chakula kisha askari wakaja wakamuuliza kama amebadili msimamo.

Alitolewa akapelekwa hoteli ya Nam, ambapo aliwakuta vijana waliofukuzwa kwenye uongozi wa Bavicha (anawataja) meya mmoja wa Mwanza na diwani aliyefukuzwa CHADEMA na kijana mwingine wa chama hicho mkoa wa Pwani aliyevuliwa uongozi wa Bavicha.
“Niliombwa nikubali kupewa sh milioni 30 ili nikubali kurekodiwa nikisema kuwa Mbowe, Dk Slaa, Lissu na Mnyika wanahusika na vitendo vya kigaidi na utekaji.

“Nilikataa. Baadaye niliingizwa katika chumba kimoja cha hoteli hiyo nikakuta mbunge mmoja wa CHADEMA kutoka Kanda ya Ziwa (anamtaja) akaniambia, ‘angalia huku’ akinionyesha simu yake kuwa alikuwa akiwasiliana na Rais,” alisema.

Kihawa aliongeza kuwa aliahidiwa kupewa cheo kizuri serikalini na fedha ili mradi akubali kuwa viongozi hao wa CHADEMA wanafanya vitendo vya kigaidi.

“Nilimuuliza kwa nini alikuwa ananishauri hivi wakati yeye ni mbunge wa chama chetu. Akasema mimi nilishinda ubunge sio kwa sababu nipo CHADEMA, bali ni muhimu hata akiondoka CHADEMA.
“Nilikataa kukubali ushauri wao ndio niliambiwa napelekwa Igunga kuunganishwa kwenye kesi ya Musa Tesha,” alisema.

Henry Kileo (Dar)
Alisema kuwa alipigiwa simu na maafisa wa polisi makao makuu Juni 17, mwaka huu, wakimwarifu kuwa wanataka kufanya mahojiano naye lakini hawakusema ni kuhusu nini.

“Juni 21, mwaka huu, wakili wangu Peter Kibatala na John Mnyika (mbunge wa Ubungo) tulienda polisi makao makuu, nilihojiwa mambo mbalimbali likiwemo tukio la kummwagiwa tindikali Musa Tesha.
“Nilicheka sana kwa kuwa kabla ya kuitwa nilipata taarifa za kikao kilichofanyika Dodoma ili kuniunganisha na kesi ya ugaidi. Mahojiano yalifanyika wakati tayari kuna kesi iliyokuwa inaendelea huko Igunga,” alisema.

Kileo alisema kuwa baada ya mahojiano hayo na kuandikisha maelezo saa 11.30 jioni, polisi walimnyima dhamana na kumpeleka rumande ya kituo kikuu cha polisi alikolala.
“Jumamosi ya Juni 22, familia yangu ilikuja kunitembelea ikakatazwa lakini baadaye wakili wangu aliwasiliana na makao makuu ya polisi ndipo wakaruhusiwa kuniona.

“Juni 22, mwaka huu, nilisafirishwa kwa ndege nikapelekwa Igunga kuunganishwa kwenye kesi ya kummwagia tindikali Musa Tesha baada ya kukataa kujibu maswali ya kuwahusisha viongozi wa CHADEMA na vitendo vya utekaji vinavyotokea nchini,” alisema.

Source: Tanzania daima

CHADEMA sasa yaupinga muswada wa sheria ya kura ya maoni ya katiba mbele ya kamati ya bunge ya katiba

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepinga muswada wa Sheria ya kura ya maoni mbele ya Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala kwa madai kuwa utakwenda kinyume na katiba ya sasa.
Chama hicho kilikuwa cha mwisho jana kutoa mapendekezo yake kati ya vyama vitano vilivyokuwapo ambavyo ni pamoja na Demokrasia Makini, Tadea, Chaumma, NLD, NRA na AFP.
Huku akitaja kesi No. 45 ya mwaka 2009 kati ya Mwanasheria Mkuu na Mchungaji Mtikila, mjumbe wa chama hicho, John Malya alisema kuwa katiba ya sasa haitambui kura ya maoni hata kama inaruhusu ushiriki wa wananchi.
Alisema ili kuwapo kwa sheria hiyo ni lazima kuibadilisha katiba ya sasa ili kuruhusu mchakato wake.
Hata hivyo mjumbe wa Katiba ya Kudumu ya Bunge ya Sheria na Katiba na Utawala ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali alisoma Katiba katika  ibara ya 98 (1b) akisema kuwa inaruhusu Bunge kutunga sheria yoyote inayoweza kubadili Katiba.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Pindi Chana alisema kuwa Chadema wana kigeugeu kwani awali walikubali kuwepo kwa kura ya maoni.
“Wakati tunapitisha muswada huu kifungu cha 6, Chadema walileta maoni tena kwenye ukumbi huu… walikubali kuwapo kwa kura ya maoni, lakini nashangaa leo wanapinga,” alisema Dk Chana.
Akijibu maoni hayo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema kuwa kifungu cha 98 cha katiba kimekuja mara ya pili kwani tangu wakati wa kuanzisha Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba kilitumika kuupinga.
“Mara ya kwanza watu walitumia kifungu cha 98 cha Katiba wakisema hakuna haja ya kuandika Katiba Mpya. Unapozungumzia kuwa Bunge linaweza kutunga sheria, ujiulize ni wabunge gani,’’ alisema.

Kesi ya Aliyejifanya kuwa mtekaji wa ulimboka yafutwa, mahakama yasema, HAHUSIKI KABISA

Ni kama Serikali imevuliwa nguo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumwachia huru raia wa Kenya, Joshua Gitu Mhindi (32), aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kutaka kumsababishia kifo, Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka. 


Hata hivyo, baada ya kuachiwa huru, alikamatwa tena na kusomewa shtaka jipya la kutoa taarifa za uongo katika kituo cha Polisi Oysterbay, kwamba alimteka nyara Dk. Ulimboka.

Mshtakiwa huyo alidaiwa kufanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha 122, cha kanuni ya adhabu.

Raia huyo wa Kenya, aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumteka na kujaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka, aliachiwa huru mbele ya Hakimu Warialwande Lema na kufunguliwa shauri jipya mbele ya Hakimu Aloyce Katemana.

Mshtakiwa huyo alisomewa shtaka hilo jipya na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, ambaye alidai Julai 3, mwaka jana katika kituo cha Polisi Oysterbay, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mulundi alitoa maelezo ya uongo kwa maofisa wa polisi, kwamba yeye pamoja na wenzake ambao hawapo mahakamani, walimtesa na kumteka nyara Dk. Ulimboka, taarifa ambazo siyo za kweli. 

Mshtakiwa huyo alikana mashtaka, na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika, na kuomba tarehe ya kutajwa pamoja na kusikiliza maelezo ya awali.

Wakili Kweka aliiambia Mahakama kuwa pamoja na kwamba dhamana kwa mshtakiwa iko wazi, Jamhuri inaomba Mahakama izuie dhamana kwa mshtakiwa huyo kwa sababu hana makazi maalum Tanzania na sababu za kiusalama kutokana na mazingira ya shauri hilo.

Alidai kwamba Mahakama ikimpa dhamana, itakuwa vigumu kwa mshtakiwa kujua tarehe ya kesi kwa sababu makazi yake hayajulikani.

Baada ya ombi hilo, mshtakiwa huyo alidai mahakamani hapo kuwa amekaa gerezani tangu mwaka jana; alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili na sasa amesomewa shtaka lingine.

“Sasa hivi wanasema nimetoa maelezo ya uongo, mheshimiwa wanataka kunipoteza nikiwa bado ni kijana mdogo, wanataka ku-silence (kunyamazisha), Bunge pamoja na wananchi,” alidai na kuongeza:

“Naumia kwa sababu nashtakiwa kwa kitu ambacho sikifahamu, mheshimiwa naenda kufanya demonstration (maandamano) na mgomo gerezani, nitachukua uamuzi ambao wewe mwenyewe utasikia.”

Hata hivyo, Mahakama ilisikiliza ombi la upande wa Jamhuri la kumnyima dhamana mshtakiwa na kurudishwa rumande hadi Agosti 20, mwaka huu.

Julai 13, mwaka jana Mhindi alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akiwa anakabiliwa na mashtaka mawili. Katika shitaka la kwanza, ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo Juni 26, mwaka jana, katika eneo la Leaders Club, alimteka Dk. Ulimboka.

Shitaka la pili, anadaiwa Juni 26 mwaka jana, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande Tegeta jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.

MBWEMBWE ZA POLISI BAADA YA KUMKAMATA
Julai 13, mwaka jana, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilimkamata Mhindi na kumfikisha Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashtaka ya utekaji nyara na shambulio la kudhuru mwili kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleman Kova, alisema mtuhumiwa alikutwa na kitambulisho cha taifa la Kenya namba 29166938 kinachoonyesha kimetolewa Oktoba, 2010 Wilaya ya Nyeri.

Pia alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na hati ya kusafiria ya dharura namba 0123431 inayoonyesha imetolewa Juni 14, mwaka jana Namanga Arusha.

Alifafanua kuwa mtu huyo alifika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe, jijini Dar es Salaam ambalo kiongozi wake ni Mchungaji Joseph Gwajima na kutaka kuonana naye bila mafanikio.

Alisema mtuhumiwa huyo alifanikiwa kuonana na Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo, Joseph Kiriba na kumweleza kuwa yeye ni mwanachama wa kikundi cha Mafia ambacho hukodiwa kufanya matukio ya kihalifu nchini Kenya na nje ya mipaka. 

Kamanda Kova alisema mtuhumiwa huyo alijiele
za alikuja Tanzania na wenzake 12, kwa lengo la kumdhuru Dk. Ulimboka, baada ya kukodiwa na mtu ambaye hakumtaja jina, lakini anaaminiwa ni mtumishi wa serikali.

Baada ya utekelezaji wa tukio hilo, wenzake waliondoka Dar es Salaam na yeye kwenda kanisani hapo kufanya toba.

Aliongeza kuwa kufuatia tukio hilo, raia wema walitoa taarifa polisi na kufanikisha kukamatwa kwa mshtakiwa huyo. 

Kamanda Kova alisema katika mahojiano ya awali mtuhumiwa huyo alidai ni mwanachama wa kikundi cha kihalifu kinachojulikana kama Gun Star, kilichopo eneo la Ruiru Wilaya ya Thika nchini Kenya. 

Alisema mtuhumiwa huyo alimtaja mmiliki wa kikundi hicho anayejulikana kwa jina la utani kama Silencer akisaidiana na Past, ambao wamemfundisha matumizi ya silaha na kwamba wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kihalifu nchini humo.

Alisema mtuhumiwa huyo alidai kuwa kati ya watuhumiwa wenzake 12, aliwafahamu wawili tu ambao alisafiri nao kutoka mjini Moshi kuja Dar es Salaam kwa ajili kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka ili ataje wanaomtuma kushawishi mgomo wa madaktari nchini.

Mtuhumiwa huyo aliliambia Jeshi la Polisi kuwa waliambiwa baada ya kukamilisha kazi waliyotumwa, wamuue Dk. Ulimboka na waliahidiwa kulipwa fedha nyingi ambazo hakuzitaja.

Kamanda Kova alisema katika mahojiano zaidi na mtuhumiwa huyo, alibainisha kuwa, Juni 26, mwaka huu walisafiri kuja Dar es Salaam kwa basi asilolikumbuka na kukutana na mwenyeji ambaye alimpeleka hoteli moja iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Ilidaiwa siku hiyo baada ya kufika walipanga namna ya kutekeleza kazi waliyotumwa kuifanya usiku huo, na kwamba alishindwa kuondoka baada ya tukio kutokana na kuona kuwa kitendo alichokifanya ni cha kinyama na kuamua kukimbilia kanisani kwa toba.

Siku chache baada ya Kova kutoa taarifa hiyo, Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Josephat Gwajima, alikana kuwa mtu huyo alikwenda kutubu kanisani hapo.

Mchungaji Gwajima alisema makanisa yote ya watu waliookoka hayana utaratibu wa waumini kutubu kwa wachungaji. 

Pia alisema mtu huyo baada ya kukamatwa, walinzi wa kanisa hilo walikubaliana na polisi wamwachie hasa baada ya yeye mwenyewe kueleza kuwa ana matatizo ya akili na hivyo amekuwa na tabia ya kuropoka ropoka hata katika mambo ambayo siyo ya kweli.

MAKINDA AZUIA MJADALA
Mwaka jana katika vikao vya Bunge, Spika Anne Makinda, alizuia mijadala ya baadhi ya wabunge waliotaka kuihoji serikali kuhusu kutekwa kwa Dk. Ulimboka kwa madai kuwa kulikuwa na kesi mahakamani.

Aidh, hatua hiyo ya kuachiwa mtuhumiwa huyo, inakuja wakati matukio ya kuteswa kwa Mhariri wa New Habari, Absalom Kibanda na mauaji ya Padre Evaristus Mushi, wa Kanisa Katoliki hajayapatiwa majibu yoyote mpaka sasa.

Aidha, uchunguzi wa matukio mawili ya milipuko ya mabomu mkoani Arusha nao haujapatiwa majibu licha ya Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi.

Tukio la kutekwa na kupigwa. Dk. Ulimboka, lilisababisha serikali kulifungia gazeti la Mwanahalisi kwa madai kuwa lilikuwa limeandika habari za uchochezi dhidi ya serikali, baada ya kutaja majina ya maofisa wa Usalama wa Taifa waliohusika na tukio hilo.

CCM yasisitiza: "Serikali tatu ni mzigo, serikali mbili safi, hata hivyo hatuwapuuzi wanaotaka tatu"


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema chama chake hakitapuuzia maoni ya WanaCCM wanaopendekeza muundo wa Serikali tatu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema: “CCM tunapendekeza muundo wa Serikali mbili, lakini hii haitufanyi tuwapuuze au tugombane na wale wenye mawazo tofauti na yetu.

“Bado tuna imani na Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, pamoja na tofauti zetu za mawazo kwa baadhi ya maeneo lakini hatuna ugomvi na tume. Tunawaheshimu sana Wajumbe wa Tume na kwa kweli tuna matumaini nao sana kuwa watatimiza wajibu wao kwa weledi mkubwa.”
Nape alisema kuwa CCM ilitangaza kujiunga kama Baraza la Katiba la kitaasisi, na kuwa baraza hili litaanzia kwenye ngazi ya tawi hadi taifa. Mpaka sasa ngazi ya matawi, wilaya na baadhi ya mikoa imeshakamilisha mchakato huo kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa vinavyotarajiwa kufanyika kati ya Agosti 20-25/08/2013 mjini Dodoma.
Alisema vikao hivyo vya kitaifa vitapokea maoni na mawazo ya wanachama, kuyapitia, kuyaunganisha na kuyaweka tayari kwa ajili ya kuyawakilisha kwa tume na kwamba CCM imeridhishwa na jinsi mchakato wa mabaraza unavyoendelea licha ya kasoro zinazojitokeza.
Nape alionya na kusema: “Hali inayojaribu kujengwa kwa nguvu si ya kweli. Tuache hoja zishindane kwa hoja na nguvu ya hoja ndiyo iwe msingi wa ushindani. Tushindanishe hoja bila kushutumiana na mwisho, mawazo ya wengi yasikilizwe na kuzingatiwa.”

Zanzibar yapendekeza mambo MATANO YA MUUNGANO YAONDOLEWEkatika rasimu ya katiba

Micheweni. Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, wametoa mapendekezo ya pamoja wakitaka mambo matano yaondolewe kwenye Muungano, yabaki kwenye Serikali washirika.
Waliyopendekeza yaondolewe ni Mambo ya Nje, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki kuu, usajili wa vyama vya siasa pamoja na ushuru wa bidhaa wakisema kwamba kama yataendelea kuwepo kwenye Muungano kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba yatasababisha Serikali shirikishi kuwa dhaifu.Wakizungumza baada ya kuwasilishwa kwa kazi za makundi yaliyopewa jukumu la kujadili suala la mihimili, wajumbe hao walisema mambo hayo matano ndiyo yanayoweza kuzipa nguvu Serikali shirikishi ambazo zitakuwa Tanganyika na Zanzibar.
Walitolea mfano wa mambo ya nje na kusema kuwa ikiwa Rais wa Serikali ya Tanganyika au Zanzibar ataondolewa jukumu la kuteua mabalozi na hata kuiwakilisha nchi nje ya nchi atakuwa ameondolewa meno. “Nchi washirika ziachiwe masuala ya mambo ya nje,”alisema Kassim Mohamed Kassi, mkazi wa Chimba akiwakilisha vijana.
Kuhusu Sarafu na Benki Kuu, walisema sababu za kupendekeza iondolewe katika muungano ni kuwa itadhoofisha uchumi wa nchi washirika.
Aidha kwa upande wa uraia na uhamiaji, walisisitiza kuwa kila nchi watu wake wana utamaduni usioingiliana na nchi nyingine washirika, hivyo kila upande uwe huru.
Ushuru wa bidhaa, wajumbe hao walipendekeza ubaki kwenye nchi washirika na siyo Muungano kama inavyopendekezwa kwa sababu ikiwa itaachwa hivyo sehemu kubwa ya kodi na ushuru kutoka nchi washirika zitashindwa kuwanufaisha watu wake.
Kuhusu usajili wa vyama vya kisiasa, wajumbe hao walisema hiyo ni moja ya kero za muungano iliyojitokeza baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi. Sheria ya chama ili kisajiliwe sharti kipate wanachama wa mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar. Walitaka mambo ya muungano yabaki mawili tu ambayo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano.

Rasimu ya katiba: CCM sasa yalumbana na KAMATI YA BUNGE YA KATIBA

Wakati maandalizi ya muswada wa sheria ya kura ya maoni wa mwaka 2013 yakianza jana jijini Dar es Salaam, kumezuka mvutano mkali kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Chama Cha Mapinduzi.
Mvutano huo umekuja wakati kamati hiyo ya Bunge ikikutana na vyama vya siasa, wasomi, asasi za kiraia na wadau wengine kwa wiki mbili mfululizo ambapo jana ilikutana na vyama vya siasa vya CCM, NCCR Mageuzi, Sauti ya Ukombozi, UPDP, huku Chadema kikiomba kwenda leo.
Mwakilishi wa CCM ambaye ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM, Joseph Tadayo ndiye alikuwa wa kwanza kutoa maoni ya chama hicho kwa kukosoa vifungu vya muswada huo likiwemo suala la muungano.
“Kifungu cha 41(3) kinachozungumzia kura za ‘NDIYO’ kina utata hasa kwa kuwa Zanzibar ni ndogo kwa Tanzania Bara, sasa ukiweka asilimia 50 kwa 50 itakuwaje? Alihoji Tadayo na kuongeza:
“Ikitokea
asilimia 99 ya Bara imesema ndiyo na asilimia moja tu ya Zanziba imesema hapana, itakuwaje? Hii ni hatari kwani tutazuia maoni ya watu.”
Alipinga pia kifungu cha 16(1) kinachoruhusu watu kupiga kampeni wakati wa kura ya maoni.
Baada ya Tadayo kutoa maoni yake, wajumbe wa kamati hiyo walianza kumuuliza maswali ambapo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alihoji kuhusu Muungano akimtaka afafanue kuhusu kura ya theluthi mbili kwa pande za muungano.
“Sheria hii itatumika kwa muungano ambao kwa Katiba ya sasa ina mambo 22. Kwa utaratibu wa sasa ili jambo liamuliwe ni lazima likubaliwe na theluthi mbili kwa kila upande, mapendekezo yenu yanaendana na katiba hii?” alihoji Lissu na kuongeza:
“Kwa kuwa Katiba ya sasa haizungumzii kura ya maoni, mnaona suala hili ni la kikatiba?”
Huku akionyesha katiba za Kenya, Zanzibar na Zimbabwe na Afrika Kusini zinazoeleza kuhusu mambo maalumu ya kupigia kura ya maoni, Lissu alimuuliza Tadayo kuhusu muswada huo kumtaka Rais kuitisha kura hiyo kwa jambo lolote lile.
Akijibu hoja hizo, Tadayo alisema hawezi kufafanua kuhusu masuala ya muungano hadi atakapowasiliana na katibu mkuu wa chama hicho na kuleta majibu kwa maandishi. ‘Tusilitazame suala la kura ya maoni kama la Muungano. Halafu siyo sahihi kusema kuwa kura hiyo haiko kikatiba. Hata kama halijatajwa katiba yetu imetoa utaratibu wa kidemokrasia,” alisema Tadayo.

Mgogoro wa ziwa nyasa; Malawi yasisitiza kuwa, ZIWA lote ni lao.......

Mashirika.  Mgombea Urais wa Democratic Progressive Party (DPP) nchini Malawi, Peter Mutharika, amesema hakuna sababu za kufanya majadiliano kuhusu Ziwa Malawi ambalo Tanzania wanaliita Ziwa Nyasa.
 Mutharika, ambaye ni mwanasheria, aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi  Mkoa wa Kati.
Akikaririwa na gazeti la  Nyasa Times, Mutharika  alisema Tanzania haina cha kuambulia kwa Ziwa Malawi.
Kiongozi
huyo ambaye hakuwapo katika mkutano wa Rais Joyce Banda na wapinzani kuzungumzia mustakabali wa ziwa, aliwahakikishia Wamalawi kuwa wasiwe na wasiwasi wa mvutano huo.
Mutharika ziwa lote ni mali ya Malawi na  akisisitiza kuwa, Tanzania haina hata punje ya eneo.
 “Hakuhitajiki majadiliano, Ziwa Malawi ni mali ya Malawi, litakuwa la Malawi,” alisema Mutharika ambaye alichukua masomo ya Sheria Tanzania.
 “Tanzania inatumia nafasi ya udhaifu wa uongozi wetu, lakini ukweli, hawana hata tone la eneo... Tutakapoitwa kwenye uchaguzi ujao mwakani, tutamaliza haya yote. Nitaleta meli nyingi kwa ajili ya maendeleo ya uchumi, kutengeneza ajira za kutosha kwa vijana,” alisema Mutharika huku akishangiliwa na wafuasi wake.
 Tanzania inataka kugawana ziwa, lakini Malawi imegomea mpango huo na suala hilo liko katika majadiliano ambayo Banda alisema kama mwafaka haukupatikana ifikapo Septemba 30, Malawi itapeleka suala hilo Mahakama ya Kimataifa (ICJ).

Wabunge wa viti maalumm wamponda SPIKA ANNE MAKINDA

Akizungumza jana kwenye mkutano wa Chama cha Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), kujadili mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya alisema wanafanya kazi nchi nzima kuwashinda wabunge waliochaguliwa.
“Mara nyingi hawa wabunge waliochaguliwa na wananchi wanalalamikiwa kwamba hawapatikani, lakini sisi wa viti maalumu muda mwingi tuko na wananchi kuangalia changamoto zinazowakabili na kuziwasilisha sehemu husika ili zitatuliwe,” alisema Bulaya. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida alisema wana michango mizuri, pia uwezo wa kuzunguka nchi nzima kutatua kero zinazowakabili wananchi. Madabida alisema kauli ya Waziri Sitta siyo sahihi akitamba kuwa wanafanya kazi na wakati mwingine kufika maeneo ambayo wabunge waliochaguliwa na wananchi hawafiki.
Hata hivyo, alitaka uandaliwe utaratibu mzuri wa kuwapata wabunge hao bila ya kujali itikadi za siasa ili watakaochaguliwa wawe ni wachapa kazi.
Mbunge mwingine wa Viti Maalumu (CCM), Ritha Kabati alisema hawaonekani kama wanafanya kazi kwa kuwa hawashirikishwi kwenye Mfuko wa Jimbo jambo linalowanyima fursa ya kutoa michango yao.
Hata hivyo, Kabati alihojiwa na gazeti hili siku chache baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa rasimu yake ikifuta viti hivyo na kusema: “Ni bora Tume ya Warioba walivyoondoa viti maalumu. Vilikuwa vinatudhalilisha, watu walikuwa hawatupi t
hamani halisi kama wabunge.” Awali, akifungua mkutano huo, Spika wa Bunge,
Anne Makinda aliwataka wabunge hao kujipanga na kutokufanya makosa kufikia uamuzi kuhusu Rasimu ya Katiba.
“Hii ni fursa ya kipekee na muhimu kwenu wabunge wanawake na Taasisi ya Bunge kwa jumla. Hatuna budi kujipanga vizuri katika kutoa maoni yetu.
“Miaka 50 baada ya uhuru, wanawake hatuna tena sababu na msamaha wa kutokushiriki kwenye zoezi hili muhimu kikamilifu... wanawake tumepata uzoefu wa kutosha, tunayo elimu ya kutosha na tunayo sauti. Kubwa zaidi ya yote tunajiamini.”
“Sisi wachache tuliokusanyika hapa tumebahatika. Ni mithili ya taa za mbele za gari ambazo ndizo humwongoza dereva wakati wa giza. Hivyo, tuna wajibu wa kuyasema matatizo na changamoto zinazowakabili wanawake na makundi mengine kama vile watoto na walemavu hususan wakati huu tunapoandika Katiba Mpya.”
“Bado kuna masuala ambayo sisi kama taasisi tungependa yaingizwe kwenye Rasimu ya Katiba. Ni vizuri tunapoandika Katiba Mpya, mihimili hii hususan Mahakama na Bunge iwiane ili kuleta heshima na kuaminiana zaidi.”

Mahakama ya TABORA yafuta mashitaka ya ugaidi dhidi ya CHADEMA

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, imefuta tuhuma za ugaidi zilizokuwa zikiwakabili makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku ikitoa tahadhari kwa wanasiasa kuepuka kulifanya suala hilo kuwa ni kitu cha kawaida katika jamii, la sivyo linaweza kusababisha madhara bila sababu.
Mbali ya kufuta shitaka hilo, Mahakama Kuu pia imesema kuwa washtakiwa Henry Kilewo na wenzake wanne, Evodius Justian, Oscar Kaijage, Seif Kabuta na Rajab Kihawa, wamebakiwa na shitaka moja ambalo ni kosa l
a kawaida la jinai, la kushambulia na kudhuru mwili. Mahakama hiyo imeamuru kwamba kesi hiyo irejeshwe na kusikilizwa Mahakama ya Wilaya Igunga, ikielezwa kuwa dhamana itakuwa wazi kwa washtakiwa.
Katika shitaka la kwanza la kesi hiyo ya marejeo Mahakama Kuu, namba 54/2013, Kilewo na wenzake, chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi, walidaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Shitaka la pili ilidaiwa kuwa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu, washtakiwa walimdhuru Tesha kwa kummwagia tindikali.
Washtakiwa hao walidaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2011, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takriban dakika 45 jana mbele ya mahakama iliyofurika watu, Jaji Mfawidhi Simon Lukelelwa, alisema suala la ugaidi siyo kitu cha mzaha au kidogo kama linavyotaka kuonyeshwa na baadhi ya watu, akionya kuwa hali hiyo ikiachwa inaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii bila sababu za msingi.
"Suala hili la ugaidi kwa siku za hivi karibuni limeshika kasi, linazungumzwa kwa mapana ndani na nje ya nchi, lakini inavyoonyesha mazungumzo hayo hayajaelewa undani wa madhara yake. Nchi ikiwa imekithiri kwa ugaidi kama inavyodaiwa, vitu vingi vingeathirika, uchumi, utalii na mambo mengine," alisema.
"Ni vizuri mambo haya yakapewa nafasi yake na kwa umakini mkubwa, yasije yakaleta madhara makubwa kwa nchi pasipo ulazima wowote. Hata neno ugaidi tafsiri yake haijajulikana vizuri, kila mtu anatafsiri zake. Mtu unayemuona wewe ni gaidi, anaweza kuwa mpigania uhuru kwa mwingine," alisema Jaji Lukelelwa akisoma hukumu hiyo.
Huku akirejea maamuzi ya kesi nyingine, Jaji Lukelelwa alisema ameridhika kuwa washtakiwa hawana hatia katika kosa la kwanza la ugaidi, huku akiwaonya waendesha mashitaka kuwa makini katika kuandaa mashitaka kwa kufuata sheria zilizopo na nyaraka za Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), zinazowaelekeza namna ya kufanya kazi zao, kwani siyo kila kosa la jinai ni ugaidi.
Katika uamuzi wake huo, Jaji Mfawidhi Lukelelwa pia alisema pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora kutokuwa na uwezo wa kusikiliza hoja za upande wa utetezi, kama zilivyoelezwa kwenye kesi namba 75/2013, kitendo cha Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Tabora, Issa Magori, kuchukua jalada la kesi hiyo ambayo haikuwa yake na kufanya uamuzi, kilikuwa ni kinyume cha sheria na taratibu za Mahakama.
Kwa mara ya kwanza watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi Juni 24, mwaka huu, wakidaiwa walimteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Upande wa serikali uliwakilishwa na Wakili Juma Massanja na Ildefons Mukandara.
Awali, watuhumiwa hao waliposomewa shitaka, jopo la mawakili wa utetezi, Abdallah Safari na Peter Kibatala, liliomba mahakama hiyo iyafute mashitaka hayo kwa sababu ya kutokuwa na uhai.
Mawakili hao wa utetezi walidai kuwa mashitaka hayo hayana uhai kwa sababu yamefunguliwa bila ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Pia mawakili hao walidai kuwa sheria za uendeshaji wa makosa kama hayo hapa nchini zinadai kuwa mashitaka kama hayo yanapofunguliwa ni lazima ridhaa ya DPP iwepo, lakini ridhaa hiyo haipo, hivyo yatupwe.
Waliongeza sababu ya pili kuwa maelezo hayaonyeshi kosa husika ni la kigaidi, tofauti na makosa mengine ya kawaida kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hivyo waliomba yafutwe au yafunguliwe kama kosa la kawaida.
Upande huo wa utetezi pia ulidai kwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya jinai, inaelekeza kuwa mshtakiwa ashtakiwe katika mahakama yenye mamlaka na hadhi kama ile waliyopelekwa katika maeneo yale walikokamatwa.
Hivyo mawakili waliiomba mahakama itupilie mbali shitaka kwani washtakiwa kama walikuwa na hatia walipaswa kushtakiwa katika maeneo yao walipokamatwa.

CHADEMA yabeza uteuzi wa msajili mpya wa vyama vya siasa, yasema, ilibidi ufanyike tangu 2008

Rais Jakaya Kikwete amemteua Jaji Francis Mutungi, kuwa Msajili mpya wa Vyama vya Siasa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari  jijini Dar es Salaam jana na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, uteuzi wa Jaji
Mutungi ulianza rasmi Agosti 2, mwaka huu.

Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ambaye amestaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.

KAULI YA CHADEMA
Kufuatia uteuzi huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema Tendwa alipaswa kuwa ameondoka kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tangu mwaka 2008 alipofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Chadema ilisema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotumwa na Ofisa Mwandamizi wa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.

Alisema Tendwa aliendelea kufanya kazi zake hata baada ya muda wa mkataba wake alioongezewa kuwa umefikia mwisho. “Hivyo, alikuwa anakalia ofisi hiyo ya umma kinyume cha sheria,” alisema Makene katika taarifa hiyo.

Alisema mbali na hilo, pia alitumia muda wa miezi kadhaa aliokuwa anakalia ofisi ya umma kinyume cha sheria, kuropoka, kuharibu demokrasia, kwa manufaa ya serikali na CCM.

Kwa mujibu wa Makene, kutokana na mwenendo wake mbovu, Chadema ilitangaza kutokumpa ushirikiano wowote, yeye kama Tendwa, ikiwa ni pamoja na kumtangaza kuwa adui wa demokrasia nchini. Hata hivyo, alisema kwa muda wote huo, Chadema ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Alisema badala ya kuifuta Chadema na kufanikisha dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye.

Hata hivyo, alisema kuondoka kwa Tendwa, hakuzuii kutekelezwa kwa mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yaliyomkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa.

Alisema kitendo hicho kilisababisha kutokea kwa mauaji yaliyofanywa dhidi ya mwandishi wa habari aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi. “Hivyo Chadema kupitia Kurugenzi ya Habari na Uenezi, inataka kauli ya Rais Jakaya Kikwete, juu ya utekelezaji wa mapendekezo hayo kwa Tendwa watu wengine, akiwamo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, 

Michael Kamuhanda, na wote waliotajwa katika ripoti hiyo ya chombo cha serikali, kuwa walivunja sheria za nchi na kusababisha mauaji ya mwandishi, raia asiyekuwa na hatia,” alisema Makene na kuongeza:

“Tunamkaribisha 'with benefit of doubt', Msajili mpya, Jaji  Francis Mutungi, kwenye kazi na majukumu yake mapya.” 

Alisema wapenda demokrasia na maendeleo nchini, wanamtarajia Jaji Mutungi kuwa atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia haki, sheria na utawala bora, na kumtaka kutopita njia ya Tendwa.
Makene alisema kupitia mchakato wa Katiba Mpya unaojadiliwa sasa hivi, Chadema inapendekeza Ofisi ya Msajili ipewe uhuru zaidi.

“Na uteuzi wake usiwe suala la Rais kuamka tu na kuamua kuteua bila wahusika kuomba, kuchujwa na kuthibitishwa na mamlaka nyingine tofauti na iliyoteua,” alisema Makene.

Hata hivyo, alisema wanatambua kuwa Mutungi aliwahi kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani kwa muda mfupi, kisha baadaye, aliteuliwa kuwa Jaji na nafasi nyingine pia. 

“Na sasa mwaka mmoja baada ya kutumikia nafasi hizo, ameteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema Makene. Kutokana na hali hilo, alimshauri Jaji Mutungi kuonyesha kwa maneno na vitendo kwamba, hatakuwa kama Tendwa. 

Alisema hiyo ni kwa kuanza kushughulikia matendo ya kiharamia yaliyofanywa na vijana wa kikundi cha ulinzi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), maarufu kama “Green Guards”. Alidai vijana hao walitenda hayo kwenye chaguzi za madiwani zilizofanyika hivi karibuni.

Makene alidai  matendo hayo si tu yalikuwa kinyume cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambayo Jeshi la Polisi linatakiwa kuchukua hatua, bali pia yalikuwa kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa. 

“Hivyo, yako kwenye mamlaka yake (Mutungi),” alisema Makene.

Alisema Jaji Mutungi alimshauri Rais Kikwete kushughulikia mapendekezo ya ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora juu ya uvunjifu wa sheria uliofanywa na askari polisi na Tendwa na kusababisha mauaji ya Mwangosi, Septemba 2, mwaka jana.

Alimtaka Jaji Mutungi kumshauri Rais Kikwete kujibu na kufanyia kazi barua mbili alizoandikiwa na Chadema juu ya kuunda Tume Huru ya Kimahakama/Kijaji, kuchunguza mauaji yaliyofanyika kwenye shughuli halali za kisiasa za Chadema.

“Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mauaji mfululizo mkoani Morogoro na Iringa, Chadema ilimwandikia barua Rais Kikwete kumtaka aunde Tume ya Kimahakama kuchunguza utata wa vifo hivyo na vingine kadhaa vilivyotokea kwenye shughuli halali za kisiasa,” alisema Makene na kuongeza:

“Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ili ukweli ujulikane, haki itendeke na wahusika wachukuliwe hatua. Hadi sasa Rais hajafanya hivyo.”

Alisema pia kuwa baada ya mlipuko wa bomu la Arusha, kwenye mkutano wa kampeni, Chadema ilimtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake kuunda Tume Huru ya Kimahakama ili ushahidi juu ya tukio hilo uwasilishwe, lakini hadi sasa pia Rais yuko kimya.

Hivyo, alimtaka Jaji Mutungi kwa nafasi yake, kumshauri Rais kuchukua hatua hizo ili vyama vitimize wajibu wa kikatiba kufanya kazi zake kwa haki, uhuru na sheria za nchi zinazosimamia shughuli za vyama vya siasa nchini.

KAULI YA CCM
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewashauri Watanzania kumpa muda Jaji Mutungi afanye kazi kwa kuwa ndiyo kwanza ameteuliwa.

Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye, alisema hayo alipotakiwa na NIPASHE jana kutoa maoni ya chama kuhusu uteuzi huo wa Jaji Mutungi.

“Ndiyo kwanza ameteuliwa. Ushauri wetu ni kwamba, mpeni muda afanye kazi halafu watu watahukumu kutokana na kazi yake,” alisema Nape

.Nipashe.
 
Support : Copyright © 2013. Tanzania Mpya - All Rights Reserved
Template Modify by Hisia za Mwananchi
Proudly powered by Hisia