Rais Jakaya Kikwete amemteua Jaji Francis Mutungi, kuwa Msajili mpya wa Vyama vya Siasa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, uteuzi wa Jaji
Mutungi ulianza rasmi Agosti 2, mwaka huu.
Mutungi ulianza rasmi Agosti 2, mwaka huu.
Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ambaye amestaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.
KAULI YA CHADEMA
Kufuatia uteuzi huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema Tendwa alipaswa kuwa ameondoka kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tangu mwaka 2008 alipofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Chadema ilisema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotumwa na Ofisa Mwandamizi wa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Alisema Tendwa aliendelea kufanya kazi zake hata baada ya muda wa mkataba wake alioongezewa kuwa umefikia mwisho. “Hivyo, alikuwa anakalia ofisi hiyo ya umma kinyume cha sheria,” alisema Makene katika taarifa hiyo.
Alisema mbali na hilo, pia alitumia muda wa miezi kadhaa aliokuwa anakalia ofisi ya umma kinyume cha sheria, kuropoka, kuharibu demokrasia, kwa manufaa ya serikali na CCM.
Kwa mujibu wa Makene, kutokana na mwenendo wake mbovu, Chadema ilitangaza kutokumpa ushirikiano wowote, yeye kama Tendwa, ikiwa ni pamoja na kumtangaza kuwa adui wa demokrasia nchini. Hata hivyo, alisema kwa muda wote huo, Chadema ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Alisema badala ya kuifuta Chadema na kufanikisha dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye.
Hata hivyo, alisema kuondoka kwa Tendwa, hakuzuii kutekelezwa kwa mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yaliyomkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa.
Alisema kitendo hicho kilisababisha kutokea kwa mauaji yaliyofanywa dhidi ya mwandishi wa habari aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi. “Hivyo Chadema kupitia Kurugenzi ya Habari na Uenezi, inataka kauli ya Rais Jakaya Kikwete, juu ya utekelezaji wa mapendekezo hayo kwa Tendwa watu wengine, akiwamo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,
Michael Kamuhanda, na wote waliotajwa katika ripoti hiyo ya chombo cha serikali, kuwa walivunja sheria za nchi na kusababisha mauaji ya mwandishi, raia asiyekuwa na hatia,” alisema Makene na kuongeza:
“Tunamkaribisha 'with benefit of doubt', Msajili mpya, Jaji Francis Mutungi, kwenye kazi na majukumu yake mapya.”
Alisema wapenda demokrasia na maendeleo nchini, wanamtarajia Jaji Mutungi kuwa atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia haki, sheria na utawala bora, na kumtaka kutopita njia ya Tendwa.
Makene alisema kupitia mchakato wa Katiba Mpya unaojadiliwa sasa hivi, Chadema inapendekeza Ofisi ya Msajili ipewe uhuru zaidi.
“Na uteuzi wake usiwe suala la Rais kuamka tu na kuamua kuteua bila wahusika kuomba, kuchujwa na kuthibitishwa na mamlaka nyingine tofauti na iliyoteua,” alisema Makene.
Hata hivyo, alisema wanatambua kuwa Mutungi aliwahi kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani kwa muda mfupi, kisha baadaye, aliteuliwa kuwa Jaji na nafasi nyingine pia.
“Na sasa mwaka mmoja baada ya kutumikia nafasi hizo, ameteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema Makene. Kutokana na hali hilo, alimshauri Jaji Mutungi kuonyesha kwa maneno na vitendo kwamba, hatakuwa kama Tendwa.
Alisema hiyo ni kwa kuanza kushughulikia matendo ya kiharamia yaliyofanywa na vijana wa kikundi cha ulinzi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), maarufu kama “Green Guards”. Alidai vijana hao walitenda hayo kwenye chaguzi za madiwani zilizofanyika hivi karibuni.
Makene alidai matendo hayo si tu yalikuwa kinyume cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambayo Jeshi la Polisi linatakiwa kuchukua hatua, bali pia yalikuwa kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
“Hivyo, yako kwenye mamlaka yake (Mutungi),” alisema Makene.
Alisema Jaji Mutungi alimshauri Rais Kikwete kushughulikia mapendekezo ya ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora juu ya uvunjifu wa sheria uliofanywa na askari polisi na Tendwa na kusababisha mauaji ya Mwangosi, Septemba 2, mwaka jana.
Alimtaka Jaji Mutungi kumshauri Rais Kikwete kujibu na kufanyia kazi barua mbili alizoandikiwa na Chadema juu ya kuunda Tume Huru ya Kimahakama/Kijaji, kuchunguza mauaji yaliyofanyika kwenye shughuli halali za kisiasa za Chadema.
“Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mauaji mfululizo mkoani Morogoro na Iringa, Chadema ilimwandikia barua Rais Kikwete kumtaka aunde Tume ya Kimahakama kuchunguza utata wa vifo hivyo na vingine kadhaa vilivyotokea kwenye shughuli halali za kisiasa,” alisema Makene na kuongeza:
“Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ili ukweli ujulikane, haki itendeke na wahusika wachukuliwe hatua. Hadi sasa Rais hajafanya hivyo.”
Alisema pia kuwa baada ya mlipuko wa bomu la Arusha, kwenye mkutano wa kampeni, Chadema ilimtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake kuunda Tume Huru ya Kimahakama ili ushahidi juu ya tukio hilo uwasilishwe, lakini hadi sasa pia Rais yuko kimya.
Hivyo, alimtaka Jaji Mutungi kwa nafasi yake, kumshauri Rais kuchukua hatua hizo ili vyama vitimize wajibu wa kikatiba kufanya kazi zake kwa haki, uhuru na sheria za nchi zinazosimamia shughuli za vyama vya siasa nchini.
KAULI YA CCM
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewashauri Watanzania kumpa muda Jaji Mutungi afanye kazi kwa kuwa ndiyo kwanza ameteuliwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye, alisema hayo alipotakiwa na NIPASHE jana kutoa maoni ya chama kuhusu uteuzi huo wa Jaji Mutungi.
“Ndiyo kwanza ameteuliwa. Ushauri wetu ni kwamba, mpeni muda afanye kazi halafu watu watahukumu kutokana na kazi yake,” alisema Nape
.Nipashe.
0 comments:
Post a Comment