Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepinga muswada wa Sheria ya kura ya maoni mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala kwa madai kuwa utakwenda kinyume na katiba ya sasa.
Chama hicho kilikuwa cha mwisho jana kutoa mapendekezo yake kati ya vyama vitano vilivyokuwapo ambavyo ni pamoja na Demokrasia Makini, Tadea, Chaumma, NLD, NRA na AFP.
Huku akitaja kesi No. 45 ya mwaka 2009 kati ya Mwanasheria Mkuu na Mchungaji Mtikila, mjumbe wa chama hicho, John Malya alisema kuwa katiba ya sasa haitambui kura ya maoni hata kama inaruhusu ushiriki wa wananchi.
Alisema ili kuwapo kwa sheria hiyo ni lazima kuibadilisha katiba ya sasa ili kuruhusu mchakato wake.
Hata hivyo mjumbe wa Katiba ya Kudumu ya Bunge ya Sheria na Katiba na Utawala ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali alisoma Katiba katika ibara ya 98 (1b) akisema kuwa inaruhusu Bunge kutunga sheria yoyote inayoweza kubadili Katiba.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Pindi Chana alisema kuwa Chadema wana kigeugeu kwani awali walikubali kuwepo kwa kura ya maoni.
“Wakati tunapitisha muswada huu kifungu cha 6, Chadema walileta maoni tena kwenye ukumbi huu… walikubali kuwapo kwa kura ya maoni, lakini nashangaa leo wanapinga,” alisema Dk Chana.
Akijibu maoni hayo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema kuwa kifungu cha 98 cha katiba kimekuja mara ya pili kwani tangu wakati wa kuanzisha Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba kilitumika kuupinga.
“Mara ya kwanza watu walitumia kifungu cha 98 cha Katiba wakisema hakuna haja ya kuandika Katiba Mpya. Unapozungumzia kuwa Bunge linaweza kutunga sheria, ujiulize ni wabunge gani,’’ alisema.
0 comments:
Post a Comment