JAMANI LULU! UMEANZA EEH!



Elizabeth Michael ‘Lulu’.
KWAKO Elizabeth Michael ‘Lulu’. Leo nimeona nikukumbuke kupitia barua! Natambua uwezo wako mkubwa katika kazi, juhudi zako binafsi ndiyo zimekufikisha hapo ulipo, mataifa mbalimbali sasa wanatambua kuwa kuna mtu anaitwa Lulu, yupo Bongo, muigizaji!.
Sitaki kukurudisha sana nyuma lakini najua unajua kuwa ni jinsi gani kipindi cha nyuma ulikuwa ukipamba vyombo vya habari kwa skendo chafu. Ulipoteza dira ya kimaisha, watu wengi waliokuwa wakikufuatilia kazi zako walianza kukutupa.
Walikupotezea kwa sababu ya matukio ya ulevi, mavazi ya nusu utupu na matukio mengi ya ajabuajabu yaliyofanana na hayo. Sina nia mbaya kukumbusha lakini waswahili wanasema binadamu anajifunza kutokana na makosa. Maishani mwako umekutana na mazito yasiyofanana na umri wako.
Kwenye ulimwengu wa mahaba, ilikuwepo minong’ono mingi juu ya watu wanaotajwa kushiriki mapenzi na wewe, walitajwa vigogo, mastaa na hata wasio mastaa. Sitaki kusema ni kweli au la lakini lisemwalo kama halipo, ujue laja.
Siri ilifichuka kupitia kifo cha yule unayedai alikuwa mwandani wako, marehemu Steven Kanumba.
Mazingira ya kifo chake, umri mdogo uliokuwa nao ilikuwa ni fundisho kubwa maishani mwako. Ulipambana na msalaba wa gereza, ukapambana na mlolongo wa kesi mahakamani hadi pale ulipofanikiwa kutoka kwa dhamana, Januari mwaka jana.
Baada ya kutoka mahabusu, kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja sasa ulikuwa kimya, ulionekana kubadilika kitabia. Yale uliyokuwa ukiyafanya awali, uliyaweka pembeni na zaidi kusimamia mustakabali mzima wa maisha yako, ulikuwa mwema sana aisee!.
Kinachonisikitisha ni kuanza kusikia tena matukio ya ajabu, unaonekana kubadilika. Nimefuatilia tabia zako, naona umeanza kubadilika, umesahau eeeh! Mavazi yako kwa miezi michache iliyopita, nimegundua yanaanza kuchepuka! Mfano mzuri ni kigauni ulichokivaa mwishoni mwa wiki iliyopita katika sherehe yako ya kuzaliwa.
Hakikustiri maungo yako nyeti, kilionesha sehemu kubwa ya matiti yako.
Kama hiyo haitoshi, kupitia mitandao ya kijamii umeanza kushusha matusi mazito bila sababu za msingi, mtu akikukosoa kidogo, unampa maneno machafu ambayo hayaandikiki gazetini. Kama kioo cha jamii, unapaswa kuvumilia mengi.
Nikiwa kwenye kazi zangu za kila siku, huwa nakuwa wa kwanza kupata fununu za mabadiliko ya kila msanii na namna anavyoishi. Nikuonye tu, kuwa makini na mwenendo wako kwani tayari jamii ilishaanza kujenga imani na wewe. Uliaminika na ndiyo maana ukapata bahati ya kuchukuliwa katika kampuni nzuri ikakusimamia kazi zako hadi sasa.
Kwa kuwa tayari nimeanza kupata malalamiko kutoka katika vyanzo vyangu, nikusihi sana mdogo wangu, usirudi ulipotoka. Jenga heshima mpya na jamii ikuamini kutokana na kazi zako na si skendo za ajabuajabu, kwa leo ni hayo tu!
Wasalam.
Ni mimi Anko Erick Evarist.
GPL

HIVI NDIVYO WAZIRI MWAKYEMBE ALIVYOUFUMUA MTANDAO WA MADAWA YA KULEVYA UWANJA WA NDEGE........

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana ameanika majina ya watu saba waliohusika kupitisha mabegi tisa yaliyokuwa na kilo 180 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh8 bilioni, Julai 5 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakiwamo maofisa usalama wanne wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na polisi mmoja.
Alisema mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, lakini siku ya tukio hilo mbwa hao walichelewa na walitumika baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.
“Kwa abiria watatu kuwa na mabegi makubwa tisa yanayofanana si kitu cha kawaida kukwepa jicho la maofisa wa ushuru wa forodha na vyombo vya usalama, sijui walikuwa wapi siku hiyo?” alihoji Mwakyembe.
Juzi waziri huyo aliahidi kuyaweka hadharani majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini, na alitekeleza ahadi hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, kusema kuwa watu hao wamenaswa baada ya mfumo wa kamera (CCTV) za uwanja huo kudaka matukio kadhaa yaliyotokea siku ya tukio hilo, kuanzia saa 9:25 hadi saa 10:30 alfajiri.
Ameagiza wafanyakazi hao wanne pamoja na askari polisi mwenye cheo cha koplo, mbeba mizigo na mfanyabiashara aliyekuwa na wasichana wawili waliokamatwa Afrika Kusini, (ambao hatuwezi kuwataja kutokana na kushindwa kuwapata kujieleza) kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kukamatwa na kuunganishwa na watuhumiwa waliokwenda na mzigo huo Afrika Kusini.
Mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya aina ya ‘Crystal Methamphetamine’, yalipitishwa na wasichana wawili wasanii aliowataja kuwa ni Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward ambao walidakwa siku hiyohiyo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini na tayari wameshafikishwa mahakamani.
Juzi Dk Mwakyembe alifanya ziara JNIA kukagua utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku tatu baada ya ahadi aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki mbili, atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege nchini.
Saa nane baada ya ziara hiyo, Maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wanadaiwa kumkamata Edwin Monyo akiwa na kete 86 za dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi aliyokuwa akiisafirisha kwenda Italia kupitia Zurich.
Mpango ulivyosukwa
Alisema siku ya tukio saa 9:28 kamera hizo za usalama zilimwonyesha mbeba mizigo wa uwanja huo akiwa anazungukazunguka eneo la kuingilia abiria kama mtu ambaye ana ahadi na kukutana na mtu fulani.
“Kamera pia zilimnasa ofisa mwingine wa TAA kwa mara kadhaa akitoka na kuingia ndani ya jengo la abiria huku akizungumza na simu, kitendo ambacho hakiruhusiwi kabisa kwa wafanyakazi wa eneo la ukaguzi wa abiria,” alisema na kuongeza;
“Wakati huohuo, kamera zilikuwa zinamwonyesha askari polisi anayetuhumiwa kuhusika katika mpango huo akiwa anarandaranda eneo la uhakiki wa hati za kusafiria kama vile anasubiri kitu fulani.”


Alisema ilipofika saa 10:15 walionekana Agnes na Melisa wakiwa na mfanyabiashara huyo katika eneo la kuingilia abiria huku wakiwa na mizigo na mabegi tisa yaliyofanana.
Alisema kuwa kamera zilimwonyesha polisi huyo akihangaika kuwasaidia abiria mbalimbali kuweka mizigo yao kwenye mashine ya ukaguzi, kazi ambayo alieleza kuwa haikuwa yake.
“Mbeba mizigo anayetuhumiwa kuwa katika mtandao huo alionekana akiwasaidia vijana hao watatu (Agnes, Melisa na mfanyabiashara) kupeleka mizigo yao kwenye mashine ya ukaguzi na baadaye kuyazungushia mabegi hayo katarasi za nailoni na kuyafikisha kaunta ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini,” alisema.
Alisema kamera hizo zilimnasa ofisa wa TAA akimwondoa katika kiti cha ukaguzi wa mizigo mfanyakazi mwenzake, na kukaa yeye ikiwa ni dakika chache kabla ya mabegi tisa ya vijana hao hayajaingia katika mashine ya ukaguzi.
“Kinyume na taratibu ofisa huyo hakujiandikisha kwenye kitabu cha wakaguzi (Screener’s logbook), saa 10:16 akaanza kupitisha mabegi hayo tisa mpaka saa 10:22. Alipomaliza kupitisha mizigo hiyo kwa dakika sita akamwachia ofisa aliyekuwa katika eneo hilo na kuondoka,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema ofisa huyo baada ya kuondoka katika kiti hicho alizungumza kwa dakika kadhaa na askari polisi anayedaiwa kuwa katika mtandao huo na kurejea tena sehemu aliyokaa ofisa mwenzake wa TAA na kumnong’oneza jambo fulani.
“Baada ya hapo akaelekea ukumbi wa abiria huku akiongea na simu, mambo hayo yote yalifanyika huku kiongozi wa sehemu ya ukaguzi akiwa hapohapo bila kushtuka,” alisisitiza.
Alisema baada ya mizigo hiyo kupita katika mashine ya ukaguzi (baggage screening machine), vijana wale watatu wakahamia na mizigo yao kwenye kaunta ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.
“Mabegi matatu ya kilo 20 kila moja yalipitishwa yakabaki mabegi sita ambayo yalitakiwa yalipiwe malipo ya uzito wa ziada. Kwa taratibu za shirika hilo kila kilo moja inayoongezeka hulipiwa dola 5 (Sh8,000), vijana wale walitakiwa kulipia dola 600, lakini walitozwa dola 94 tu ambazo zinathibitishwa na risiti tuliyonayo,” alisema.
Alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida mfanyabiashara ambaye hakuwa na tiketi ya kusafiri siku hiyo, baadaye alibadili mawazo hapohapo na kuamua kuondoka siku hiyo kwenda Afrika Kusini na kulipia gharama ya dola 60 (Sh96,000) ili kupata tiketi.
“Kutokana na hali hiyo mhakiki wa nyaraka za safari nje ya ukumbi wa abiria siku hiyo, hakupaswa kumruhusu mfanyabiashara kuingia ndani ya ukumbi bila tiketi ya siku hiyo,” alisema na kuongeza;
“Kwa hali ya kawaida mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa, lakini siku hiyo mbwa walichelewa na walikuja kutumika baadaye ikiwa ni baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.”

Hatua za wizara
Alisema wizara imeagiza TAA kuwa, kuanzia sasa mtu yeyote anayekamatwa na dawa za kulevya lazima apigwe picha na zisambazwe kwenye vyombo vya habari.
Pia ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kumkamata mfanyabiashara anayedaiwa kuwasaidia Masogange na mwenzake kusafirisha dawa za kulevya ambaye alitoweka na mabegi matatu ya dawa hizo huko Afrika Kusini, “Akamatwe na kuunganishwa na kesi inayowakabili Watanzania hao wawili.”
Alisema mbeba mizigo anatakiwa kufukuzwa kazi na mwajiri wake na asiruhusiwe kukanyaga JNIA, kwamba serikali imewaagiza polisi kumkamata mtu huyo kwa lengo la kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka ya jinai chini ya sheria ya kuzuia dawa za kulevya, sura ya 95 ya mwaka 1996.
Alisema TAA inatakiwa kuwafukuza kazi mara moja wafanyakazi wake wanne waliohusika katika mpango huo, kuwakamata na kuwaunganisha katika mashtaka yanayowakabili.
“Jeshi la polisi limeagizwa kumwondoa mara moja askari mwenye cheo cha koplo anayedaiwa kuhusika katika tukio hilo na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwa njia moja au nyingine kwenye njama za kupitisha mabegi hayo ya dawa za kulevya,” alisema.
Alifafanua kuwa Idara ya Usalama wa Taifa imeagizwa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu siku ya tukio kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wakati mwafaka, jambo ambalo limeliletea taifa fedheha kubwa.
“Serikali imeziagiza taasisi zote zilizopo chini ya JNIA kutekeleza majukumu ipasavyo na kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kuhakikisha dawa za kulevya hazipiti kwenye kiwanja hicho kikuu cha ndege nchini,” alisisitiza.

BAKWATA sasa yamuunga mkono PONDA, yawaponda POLISI..........

 Baraza la waislamu Tanzania BAKWATA limeitaka serikali kuunda tume huru ya uchunguzi na kumtaka kamanda wa polisi mkoani Morogoro Faustine Shilogile kujiuzulu ili kupisha tume hiyo itakayoundwa kulifanyia uchunguzi madai ya tukio la katibu wa jumuia na taasisi za Kiislamu nchini shekhe Ponda Issa Ponda kupigwa risasi na polisi mkoani humo huku familia yake ikitoa msimamo wao kuhusiana na tukio hilo.
Msimamo huo wa BAKWATA umetolewa na sheikh mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum katika makao makuu ya mkoa ya baraza hilo na kuongeza kuwa licha ya Bakwata kutofautiana kifikra na Sheikh Ponda hawaungi mkono kwa namna yeyote ile tukio hilo la madai ya kupigwa risasi na polisi huku akilitaka jeshi la polisi nchini kujipanga upya katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuepuka matumizi makubwa ya nguvu ikiwa ni pamoja na kutumia risasi za moto kwa raia kwa kuwa hali hiyo inachafua sura na amani ya nchi iliyopo hivi sasa na kuwataka wote waliohusika katika tukio hilo kuwajibishwa.
Sheikh Alhad ameonya kuwa endapo itathibitika pasi na shaka kuwa sheikh Ponda amedhuriwa kwa risasi ya moto na jeshi la polisi ni dhahiri kuwa mahusiano mema baina ya raia hasa wa jamii ya kiislamu na polisi yatakuwa ni ya mashaka.
Akizungumza na vyomba vya habari katika taasisi ya tiba ya mifupa na upasuaji wa mishipa ya fahamu, MOI meneja uhusiano wa MOI Juma Almas amekiri sheikh Ponda kulazwa hospitalini hapo na kwamba imekuwa ni vigumu kujua majeraha aliyo nayo yamesababishwa na kitu gani kwa kuwa majeruhi alifikishwa katika taasisi hiyo akiwa tayari ameshashonwa jeraha.
Katika taasisi ya tiba ya mifupa na upasuaji wa mishipa ya fahamu,moi alikolazwa sheikh ponda issa ponda ambapo itv imemtembelea na kuonana nae licha ya kutozungumza lolote msemaji wa familia hiyo amesema wanapata mashaka kutokana na kile alichokiita kuwa ni upotoshaji wa makusudi unaofanywa kuficha sababu za sheikh Ponda kuumizwa na kusema kile familia inachoamini kimemdhuru sheikh Ponda.
Katika eneo hilo la wodi alikolazwa sheikh Ponda kumeonekana uwepo wa ulinzi mkali ambapo ITV imeshuhudia askari kanzu pamoja na baadhi ya askari waliokuwa na silaha wakilinda eneo lote la wodi hiyo.
 
source ITV TZ

SAKATA LA KUMWONDOA MEYA: CCM hoi Bukoba, Madiwani wapewahongo, watishiwa kufukuzwa uanacham

HATUA ya madiwani wanane wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika manispaa ya Bukoba, kusaini hati ya tuhuma na kuiwasilisha barua hiyo kwa mkurugenzi wa manispaa hiyo, kumtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kutokuwa na imani na meya anayetuhumiwa kujiingiza katika miradi ya kifisadi imechukua sura mpya.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana jioni kutoka mjini Bukoba, zilisema kuwa msimamo huo umewagawa viongozi wa CCM mkoa wa Kagara na hivyo kuitisha kikao cha halmashauri ya mkoa leo kwa ajili ya kuwajadili na kuwafukuza madiwani hao.
Hata hivyo uamuzi huo, huenda ukakigharimu chama hicho kutokana na madiwani hao kusisitiza msimamo wao, wakisema wako tayari kufukuzwa kwa sababu wanatetea maslahi ya wananchi wakipinga ufisadi.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili kwa masharti ya kuhifadhiwa jina lake, mmoja wa madiwani hao alisema kuwa rushwa imekuwa ikitembezwa waziwazi kwa wajumbe wa vikao mbalimbali vya CCM ili kuwalazimisha wakutane mara kwa mara kufikia uamuzi huo.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa katika kuwagawa madiwani hao ambao wameungana na wenzao wa vyama vya CHADEMA na CCM ili kupunguza idadi ya akidi, diwani mmoja alijaribiwa kuhongwa milioni 20 ili aondoe jina lake katika orodha hiyo.
“Mwenzetu mmoja kwa kweli amekuwa jasiri wa ajabu, juzi aliitwa mahala akatumiwa watu wakiwa na fedha taslimu milioni 20 lakini alikwepa mtego huo na kuwakimbia watu waliotumwa, akisisitiza kuwa hawezi kutusaliti. Sasa kwa hali hii kama CCM wanadhani wanaweza kukinusuru chama kwa kutufukuza na wajaribu waone,” alisema.
Naye diwani mwingine alidokeza kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wilaya na mkoa ndio wanatumika kuwarubuni madiwani hao kwa rushwa ili waondoe tuhuma hizo dhidi ya meya, Anatory Amani.
Hivi karibuni, madiwani hao walimgeuka Rais Jakaya Kikwete, wakipinga uamuzi wake wa kumtaka meya kumaliza tofauti zake na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwa kile walichodai mgogoro huo si ugomvi kati ya wawili hao.
Madiwani hao walipinga kauli hiyo wakisema suluhu ni kupinga ufisadi wa meya, kwani hakuna ugomvi binafsi kati yake na mbunge.
Akihutubia mkutano mjini Bukoba, Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo lazima uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano “yasiyokuwa na msingi”.
Madiwani hao 15 walisema malumbano yaliyopo ni ya msingi kwa kuwa watu watakaobebeshwa deni la kurejesha mikopo inayochukuliwa na meya ni wakazi wa Bukoba, si meya mwenyewe.
Walisema Rais ameonekana hafahamu kiini cha mgogoro, kwani kinachopingwa si miradi, bali utaratibu ambao meya ametumia kuanzisha miradi hiyo kifisadi bila kuzingatia maslahi ya wananchi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Barua ya madiwani hao, iliwasilishwa jana asubuhi saa 2.30 na kupokelewa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Shimwela L.E, ikiwa na saini za madiwani 16 kati ya 24 waliopo.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo, alipotafutwa na gazeti hili alishindwa kukiri au kukanusha kupokea barua hiyo, akisingizia kuwa kwa muda huo alikuwa akitekeleza majukumu yake nje ya ofisi.
“Unajua Rais juzi aliacha maagizo mengi na baya zaidi ni lile la ugawaji wa viwanja, hivyo asubuhi niliingia ofisini na kutoka kuelekea mitaani. Nitakupa taarifa kesho kama barua hiyo imefika,” alisema.
Kwa mujibu wa kanuni za manispaa hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM, ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.
Kanuni hizo pia zinaelekeza kuwa mkugenzi atapaswa kuitisha kikao hicho ndani ya siku saba kuanzia tarehe aliyopokea barua ya tuhuma hizo za madiwani na ndani ya muda huo anapaswa kuwa amempatia mtuhumiwa tuhuma hizo ili aweze kuzijibu.
Alisema walikuwa wamesaini madiwani 16 lakini waliamua kumtoa Balozi Kagasheki kwa vile ni waziri na sehemu ya serikali, hivyo walibakia madiwani 15. Hata hivyo, inajulikana kuwa hata Kagasheki anawaunga mkono itakapofika hatua ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.
Madiwan hao wanaompinga meya ni Richard Gaspar (CCM), Rabia Badru (CUF), Murungi Kichwabuta (CCM), Winfrida Mukono (CHADEMA), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (CCM), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Deusdedit Mutakyahwa (CCM), Robert Katunzi (CCM), Samwel Ruhangisa (CCM) na Dauda Kalumuna (CCM).
Wengine ni Dismas Rutagwelela, Israel Mlaki wa CHADEMA na Conchester Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho pamoja na Ibrahim Mabruk, Felician Bigambo wa CUF.

source: Tanzania daima

"MZUNGU" AKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI ZENYE THAMANI YA ZAIDI YA SH.MILIONI 100

RAIA wa Uingereza, Robert Dewar, amekamatwa na nyara za serikali zenye thamani ya sh 118,314,900 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, mtuhumiwa huyo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trans Afrikas Logistics (TALL), akikamatwa Agosti 9, mwaka huu, akiwa na nyara hizo.
Alizitaja nyara hizo kuwa ni vipande vinane vya meno ya tembo, vinyago 11, meno ya tembo 20, meno 20 na kucha 22 za Simba, ndege mmoja aina ya kasuku, vipande vya miti ya mpingo na idadi kubwa ya vinyago, vyote vikiwa na uzito wa kilogramu 24.
Mtuhumiwa huyo pia alikutwa akiwa na mawe yanayodhaniwa kuwa ni madini pamoja na ganda moja la bomu lenye ukubwa wa milimita 130.
Kamishna Kova aliongeza kuwa mtuhumiwa amekuwa akisafirisha vitu hivyo sehemu mbalimbali duniani, na kwamba atafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limeahidi zawadi nono ya sh milioni 100 kwa mtu atakayetoa au kufanikishwa kukamatwa wahalifu wanaotuhumia kutumia tindikali kuwadhuru watu mbalimbali.
Kamishna Kova alisema kuwa matukio hayo yamekithiri nchini, ikiwamo tukio la raia wa Lebanon ambaye ni Mkurugenzi wa Home Shopping Centre jijini Dar es Salaam kumwagiwa kemikali iliyomletea madhara makubwa.
Katika hatua nyingine, watu wawili wamesomewa shitaka katika Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Ilala wakikabiliwa na tuhuma za wizi wa kutumia silaha.
Washtakiwa hao, Abdalla Shamte (30) na Mussa Hassan (40) wanadaiwa kuiba mabati 47 na vipande 11 vya mbao, vyenye thamani ya sh 3,084,000 mali ya Dk. Justine Paul.
Washtakiwa wote walikana kosa hilo lilisomwa na Mwendesha Mashtaka, Munde Hamisi, mbele ya Hakimu Joyce Minde.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 26, mwaka huu na washtakiwa walipelekwa rumande.

source: Tanzania daima
 
Support : Copyright © 2013. Tanzania Mpya - All Rights Reserved
Template Modify by Hisia za Mwananchi
Proudly powered by Hisia