Wakati bilionea mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite
yanayopatikana Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara,
marehemu Erasto Simon Msuya (43) akitarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwao
mtaa wa Kairo, Mji mdogo wa Mirerani, polisi imewatia mbaroni watu
wawili wakihusishwa katika mtandao uliofanya mauaji ya mfanyabiashara
huyo.
Mfanyabiashara huyo anayemiliki vitega uchumi
kadhaa katika miji hiyo, aliuawa Agosti 8, mwaka huu katika eneo la
Mjohoroni wilayani Hai baada ya kumiminiwa risasi zaidi ya 20 za bunduki
ya kivita aina ya SMG.
Habari zilizopatikana jana Arusha, zilidokeza kuwa
washukiwa hao walikamatwa siku ya tukio huko Sanyajuu wilayani Siha,
kilomita chache kutoka mahali ilipotelekezwa pikipiki iliyotumika katika
mauaji hayo.
Pikipiki hiyo mpya ilitelekezwa katika Kijiji cha
Olkolili baada ya kupata pancha gurudumu la mbele na watu waliokuwa
wakiitumia waliiacha na kuamua kutembea kwa miguu.
Habari zinadai kuwa watu hao wawili sio
waliomfyatulia risasi mfanyabiashara huyo bali wana ‘taarifa muhimu’
zinazohusiana na mpango mzima wa mauaji hayo na mtandao wa watuhumiwa
waliohusika.
Inadaiwa kuwa baada ya wauaji wa mfanyabiashara
huyo kutelekeza pikipiki hiyo, ‘waliwezeshwa’ kutoroka kupitia Wilaya ya
Simanjiro na baadaye kuingia jijini hapa ingawa hawajulikani mahali
waliko.
“Ni kweli kuna watu wawili walikamatwa na
wanashikiliwa kule Makao Makuu ya Polisi Moshi na kila siku wanaletwa
hapa Arusha kwa ajili ya uchunguzi wa kuwatafuta wahusika hasa,”
alidokeza polisi mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuelezea zaidi baada ya simu yake kutokupatikana.
Ofisa huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe,
alisema hata hiyo jana, timu ya wapelelezi kutoka Moshi wakiongozwa na
RCO Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi walikuwapo jijini hapa na watuhumiwa
hao.
Uchunguzi zaidi wa polisi kuhusu mmiliki halali wa
pikipiki iliyokuwa ikitumiwa na vijana wawili waliotekeleza mauaji
hayo, zimebaini kuwa bado inamilikiwa na kampuni moja ya Dar es Salaam
iliyouza pikipiki hiyo.
Habari zaidi zinadai kuwa pikipiki hiyo
ilinunuliwa mahususi kwa ajili hiyo na mwanamke mmoja ambaye hafahamiki
na ilinunuliwa katika duka ambalo ni tawi la kampuni iliyoingiza
pikipiki hiyo lililopo Arusha.
Mfanyabiashara huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa
kesho, huko Mirerani, aliuawa baada ya kuitwa kwa simu na wauaji
waliojifanya ni vijana wenye madini ya Tanzanite waliotaka kumuuzia
marehemu.
Alisema ameacha mke na watoto wanne, wawili wa kike na wawili wa
kiume na ameacha rasilimali nyingi zikiwamo nyumba ya
kifahari,migodi,hoteli maarufu za SG Resort na Mezza Luna zilizopo
Arusha.
Pia, ameacha magari mengi ya kifahari ikiwemo
Range Rover Vogue (New Model) ambalo alikuwa nalo wakati akipigwa risasi
kwenye eneo la mijohoroni (kwa wasomali) kati ya Boma ng’ombe wilayani
Hai na uwanja wa ndege wa Kia.
Hata
hivyo, marehemu alipofika eneo hilo akiwa na gari lake la kifahari aina
ya Range Rover toleo jipya, alishuka kwenda kuzungumza na vijana hao
mita kama 70 kutoka kwenye gari lake na ndipo alipomiminiwa risasi.
Inadaiwa kuwa baada ya vijana hao kumuua,
walichukua begi jeusi lililokuwa na fedha ambazo angezitumia kununulia
madini hayo lakini hawakuchukua simu wala bastola ya marehemu
anayoimiliki kihalali.
Kumekuwapo na taarifa zinazotatanisha kuhusu kiasi
hasa kilichoibwa huku taarifa zikidai ni Sh50 milioni na nyingine
zikidai ni Sh120 milioni.
Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Robert Boaz alikaririwa na gazeti hili akikanusha taarifa
kuwa ndani ya gari la marehemu kulikuwapo na kiasi cha fedha Sh150
milioni kilichokutwa.
Mazishi kufanyika kesho
Akizungumza na gazeti hili jana, Shujaa Godfey
ambaye ni shemeji wa marehemu Msuya, alisema mwili wa marehemu
umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre
(Seliani) na mazishi yatafanyika kesho.
Shujaa alisema mtoto mkubwa wa marehemu, Simon
Erasto ambaye anasoma nchini Australia, aliwasili jana Jumapili kwa
ndege baada ya kutua Dar es Salaam na kupanda tena ndege iliyomshusha
Kia kwa ajili ya kushiriki mazishi kesho.
“Kabla ya kifo chake, marehemu Msuya aliacha wosia
kuwa azikwe mtaa wa Kairo na misa ya mazishi yake ifanyike kwenye
Kanisa la Lutherani lililopo Kairo ambalo alichangia nguvu kubwa katika
kulijenga,” alisema Shujaa.
Kifo cha Msuya kilichotokea Jumatano iliyopita ya
Agosti 7 mwaka huu, kwa kuuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20, kiliacha
gumzo kwenye miji ya Arusha Moshi na Mji mdogo wa Mirerani ambapo ndipo
nyumbani kwao.
Katika mazishi ya kesho, watu mbalimbali maarufu
nchini wanatarajia kushiriki wakiwamo wa chama na Serikali, wabunge na
viongozi wa vyama vya kisiasa kwani enzi za uhai wake Msuya alikuwa kada
maarufu wa CCM.
Shujaa alisema marehemu Msuya alizaliwa mwaka 1970
huko Shighatini wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro na alipata elimu ya
msingi shule ya Shighatini mwanzoni mwa miaka ya 80 na mwanzoni mwa
miaka ya 90 akajiunga na Shule ya Sekondari Makumira iliyopo mji mdogo
wa Usa River wilayani Arusha kwa kidato cha nne na kisha akajiunga na
Shule ya Sekondari Tanga kwa kidato cha sita.
“Mwishoni mwa miaka ya 90 alichaguliwa kujiunga na
Chuo Kikuu Dar es salaam kusomea Shahada ya Uchumi ila aliacha kwenda
na akawa anajishuhulisha na uchimbaji na ununuzi wa madini,” alisema
Shujaa.
0 comments:
Post a Comment