RAIA wa Uingereza, Robert Dewar, amekamatwa na nyara za serikali zenye thamani ya sh 118,314,900 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, mtuhumiwa huyo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni
ya Trans Afrikas Logistics (TALL), akikamatwa Agosti 9, mwaka huu, akiwa
na nyara hizo.
Alizitaja nyara hizo kuwa ni vipande vinane vya meno ya tembo, vinyago
11, meno ya tembo 20, meno 20 na kucha 22 za Simba, ndege mmoja aina ya
kasuku, vipande vya miti ya mpingo na idadi kubwa ya vinyago, vyote
vikiwa na uzito wa kilogramu 24.
Mtuhumiwa huyo pia alikutwa akiwa na mawe yanayodhaniwa kuwa ni madini
pamoja na ganda moja la bomu lenye ukubwa wa milimita 130.
Kamishna Kova aliongeza kuwa mtuhumiwa amekuwa akisafirisha vitu hivyo
sehemu mbalimbali duniani, na kwamba atafikishwa mahakamani upelelezi
ukikamilika.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limeahidi zawadi nono ya sh
milioni 100 kwa mtu atakayetoa au kufanikishwa kukamatwa wahalifu
wanaotuhumia kutumia tindikali kuwadhuru watu mbalimbali.
Kamishna Kova alisema kuwa matukio hayo yamekithiri nchini, ikiwamo
tukio la raia wa Lebanon ambaye ni Mkurugenzi wa Home Shopping Centre
jijini Dar es Salaam kumwagiwa kemikali iliyomletea madhara makubwa.
Katika hatua nyingine, watu wawili wamesomewa shitaka katika Mahakama
ya Mwanzo ya Wilaya ya Ilala wakikabiliwa na tuhuma za wizi wa kutumia
silaha.
Washtakiwa hao, Abdalla Shamte (30) na Mussa Hassan (40) wanadaiwa
kuiba mabati 47 na vipande 11 vya mbao, vyenye thamani ya sh 3,084,000
mali ya Dk. Justine Paul.
Washtakiwa wote walikana kosa hilo lilisomwa na Mwendesha Mashtaka, Munde Hamisi, mbele ya Hakimu Joyce Minde.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 26, mwaka huu na washtakiwa walipelekwa rumande.
source: Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment