Baraza la waislamu Tanzania BAKWATA limeitaka serikali kuunda tume
huru ya uchunguzi na kumtaka kamanda wa polisi mkoani Morogoro Faustine
Shilogile kujiuzulu ili kupisha tume hiyo itakayoundwa kulifanyia
uchunguzi madai ya tukio la katibu wa jumuia na taasisi za Kiislamu
nchini shekhe Ponda Issa Ponda kupigwa risasi na polisi mkoani humo huku
familia yake ikitoa msimamo wao kuhusiana na tukio hilo.
Msimamo huo wa BAKWATA umetolewa na sheikh mkuu wa
mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum katika makao makuu ya mkoa ya
baraza hilo na kuongeza kuwa licha ya Bakwata kutofautiana kifikra na
Sheikh Ponda hawaungi mkono kwa namna yeyote ile tukio hilo la madai ya
kupigwa risasi na polisi huku akilitaka jeshi la polisi nchini kujipanga
upya katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuepuka matumizi
makubwa ya nguvu ikiwa ni pamoja na kutumia risasi za moto kwa raia kwa
kuwa hali hiyo inachafua sura na amani ya nchi iliyopo hivi sasa na
kuwataka wote waliohusika katika tukio hilo kuwajibishwa.
Sheikh Alhad ameonya kuwa endapo itathibitika pasi
na shaka kuwa sheikh Ponda amedhuriwa kwa risasi ya moto na jeshi la
polisi ni dhahiri kuwa mahusiano mema baina ya raia hasa wa jamii ya
kiislamu na polisi yatakuwa ni ya mashaka.
Akizungumza na vyomba vya habari katika taasisi ya
tiba ya mifupa na upasuaji wa mishipa ya fahamu, MOI meneja uhusiano wa
MOI Juma Almas amekiri sheikh Ponda kulazwa hospitalini hapo na kwamba
imekuwa ni vigumu kujua majeraha aliyo nayo yamesababishwa na kitu gani
kwa kuwa majeruhi alifikishwa katika taasisi hiyo akiwa tayari
ameshashonwa jeraha.
Katika taasisi ya tiba ya mifupa na upasuaji wa
mishipa ya fahamu,moi alikolazwa sheikh ponda issa ponda ambapo itv
imemtembelea na kuonana nae licha ya kutozungumza lolote msemaji wa
familia hiyo amesema wanapata mashaka kutokana na kile alichokiita kuwa
ni upotoshaji wa makusudi unaofanywa kuficha sababu za sheikh Ponda
kuumizwa na kusema kile familia inachoamini kimemdhuru sheikh Ponda.
Katika eneo hilo la wodi alikolazwa sheikh Ponda
kumeonekana uwepo wa ulinzi mkali ambapo ITV imeshuhudia askari kanzu
pamoja na baadhi ya askari waliokuwa na silaha wakilinda eneo lote la
wodi hiyo.
0 comments:
Post a Comment