Home » » WAKULIMA waaswa kutumia vizuri fursa za maaonesho ya NANENANE

WAKULIMA waaswa kutumia vizuri fursa za maaonesho ya NANENANE

SHEREHE za wakulima maarufu kama Nane Nane zimekuja wakati mwafaka, ambapo wakulima na sekta ya kilimo imekuwa ikikabiliwa mabadiliko ya tabia nchi, ikiwamo ukame.
Mbali na hili, pia kilimo kinakabiliwa na pembejeo feki ambazo wakulima wanauziwa, hivyo kupata hasara ikiwamo mazao kidogo na hafifu.
Maonyesho haya yanayofanyika mkoani Dodoma yatawasaidia wakulima kupata elimu juu ya pembejeo halisi ikiwamo mbegu, dawa (viuatilifu), mbolea kutoka kwa mashirika husika yanayozalisha pembejeo mbali mbali, ili kuwasaidia kuepuka kununua pembejeo feki ambazo huwasababishia hasara na kuwakatisha tamaa.
Sherehe hizi huambatana na maonyesho ya bidhaa za kilimo yanayofanywa na wakulima na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya kilimo, lengo likiwa ni kujitangaza shughuli zao, kubadilishana uzoefu na wataalamu wa kilimo.
Pia wakulima wadogo ambao ni wengi ukilinganisha na wakulima wakubwa watajifunza mbinu mpya za kitaalamu za kilimo zinazoendana na wakati tulionao sasa kwa maana ya mabadiliko ya kiteknolojia na tabia nchi ili wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa na kunufaika kiuchumi.
Kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea ambacho hakizingatii kanuni za kitaalamu, jambo lililowasababisha kukata tamaa na kuona kuwa kilimo hakilipi kutokana na mbinu duni walizozitumia.
Mkulima John Mwenda anayetarajia kunufaika na maonyesho hayo, anasema tangu mwaka 2009 amekuwa akipata elimu ya kilimo katika maonyesho ya Nane Nane ambayo yamemsaidia kufanya kilimo chenye manufaa kiuchumi.
Anasema wakati ndio huu kwa wakulima kuamua kujifunza mbinu mpya za kilimo zitakazowawezesha kupata mazao mengi na kutimiza ndoto zao.
“Kilimo kisiwe tu kwa ajili ya chakula bali kiwasaidie kujikimu na kuondokana na umaskini.
“Wakulima waondokane na kilimo cha kubahatisha cha kutegemea mvua na badala yake wajikite katika kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika, kinachoweza kuyabadilisha maisha ya mkulima kiuchumi kutokana na mazao mengi atakayoyapata,” anasema.
Ni wazi kwamba mvua zimekuwa haziendani na kalenda ya wakulima, na hilo ni tatizo kwa sababu mazao yamekuwa yakinyauka.
Sekta ya kilimo inapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu kutokana na umuhimu wake katika nchi na ustawi wa jamii, ni sekta ambayo imeajiri watu wengi zaidi kuliko sekta nyingine.
Takwimu zilizofanyika zinaonesha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanategemea sekta ya kilimo kama ajira yao.
Sehemu kubwa ya kilimo ni cha wakulima wadogo wadogo ambao mashamba yao yana ukubwa wa hekta 0.9 na hekta 3.0 kwa kila moja.
Karibu asilimia 70 ya ardhi ya kilimo na mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 hutumia maksai na asilimia 10 hutumia trekta.
Mbali na hayo, kilimo cha Tanzania ni cha kutegemea mvua, uzalishaji wa mazao ya chakula ndio unaongoza katika uchumi wa kilimo.
Hekta milioni 5.1 zinalimwa nchi nzima kila mwaka, kati ya hizo asilimia 85 ni kwa a
jili ya mazao ya chakula tu, na wanawake ndio wafanyakazi wakubwa mashambani.
Kilimo chetu kinakabiliwa na matatizo au changamoto mbalimbali zikiwamo matumizi duni ya pembejeo kama mbegu bora na mbolea, idadi kubwa ya wakulima na wafugaji kutokupata huduma za kutosha za ugani, elimu na ufahamu mdogo kuhusu teknolojia mpya zitolewazo na taasisi za tafiti, uhaba na ukosefu wa masoko ya mazao ya wakulima.
Vilevile kutokuongezwa thamani ya mazao yetu ya kilimo na mifugo, miundombinu duni hasa barabara za kufikia masoko vijijini na pia maghala au sehemu salama za kuhifadhi mazao yao na ukame na wakati mwingine mafuriko kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Joel Melau ni mkulima katika Wilaya ya Arumeru anayependekeza maonyesho ya Nane Nane yatumike kuwaunganisha wakulima ili wawe na umoja na sauti moja katika soko la sivyo wakulima wataendelea kulanguliwa na kulubuniwa na wafanyabiashara wanaoyanunua mazao yao kwa bei ndogo.
Hali hiyo anasema inawasabaishia wakulima kutonufaika na kilimo chao kama inavyotakiwa, wanaofaidika wanabakia kuwa walanguzi na madalali wanaotegemea wakulima kuwanyonya.
Baada ya kuimarisha umoja na ushirikiano wa wakulima wenyewe ni vema wakulima wakajenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara ili kutokutoa mianya kwa madalali ambao mara nyingi wamekuwa wakilalamikiwa kuwa wananunua mazao ya wakulima kwa bei ya chini huku wakiyauza kwa bei ya juu.
Ni vema kukatengenezwa mfumo mzuri utakaowasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za masoko na bei halisi ya bidhaa kupitia umoja wao, kuliko kuendelea kusherehekea kila mwaka wakati wakulima bado wanateseka na bei kandamizi za madalali.
Suala hili linaenda sambamba na kaulimbiu ya sherehe za Nane Nane mwaka huu ambayo ni“Zalisha mazao ya kilimo na mifugo kwa kulenga mahitaji ya soko.”
Wakulima hawawezi kuyajua mahitaji ya masoko wasipopata taarifa sahihi za masoko kwani wataendelea kulima kwa mazoea na mazao yao yataendelea kuozea ghalani.
Bado wakulima wanaendelea kuilaumu serikali juu ya kuzuiwa kuuza mazao yao nje ya nchi ambapo wanadai kuwa wanayauza kwa bei nzuri na ya faida tofauti na soko la ndani.
Wakulima hawa wanahisi kama wanaonewa kwa sababu wanalima kwa gharama zao wenyewe na bado wananyimwa kuuza nje ya nchi.
Ni vizuri kukawa na mikakati mizuri ya kuwatafutia wakulima wetu masoko ya uhakika na kwa bei stahiki ili kuondokana na malalamiko haya.
Inashangaza kuona sehemu moja ya nchi inakabiliwa na uhaba wa chakula huku sehemu nyingine mazao yakiozea ghalani kwa kukosa soko, kweli hii ni haki?
Hapa utaona kabisa hakuna kiunganishi kizuri kati ya wakulima na soko, jambo linalowakatisha tamaa wakulima kuona kuwa licha ya juhudi wanazozifanya kuzalisha chakula kingi bado serikali haiwajali kama inavyotakiwa, japo mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia kwa kiasi fulani, lakini je, wamefika maeneo yote ya nchi?
Sherehe hizi ziwe chachu ya kujadili na kutathmini maendeleo ya sekta ya kilimo na changamoto zinazowakabili wakulima na kuangalia namna ya kuzitatua.
Ikiwa zimesalia siku chache kufikia kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima, maarufu kama Nane Nane, tayari maandalizi mbalimbali yamefanyika likiwamo suala la uboreshaji miundombinu, nishati ya umeme pamoja na maji ili kuhakikisha maonyesho hayo yatawavutia watu wengi na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Akizungumzia maandalizi hayo, Katibu wa Chama cha Kilimo (TASO) ambao ndio waandaaji wa maonyesho hayo, Peter Ngasa, anasema katika suala la uboreshaji wa miundombinu wameweza kujenga barabara kwa kiwango cha tofali ili watu wasiweze kupata adha ya vumbi, pia katika suala la umeme wameongeza transfoma moja ili kuhakikisha nishati inakuwapo kwa kipindi chote cha maonyesho hayo.
“Pia katika suala la maji tumeongeza visima viwili na suala la usafi wa viwanja limezingatiwa kama unavyoona shughuli za usafi bado zinaendelea,” anasema.
Katibu huyo anasema wanatarajia wakulima watajifunza mbinu bora za kisasa za kilimo zitakazowawezesha kupata mazao mengi na kuinua kipato chao.
Ngasa anatoa wito kwa wakulima na mashirika kujitokeza katika maonesho hayo kwa sababu watapata fursa ya kujifunza mambo mengi na kubadilishana uzoefu na wataalamu mbalimbali wa kilimo.
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan Tanzania Mpya untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Hisia za Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Copyright © 2013. Tanzania Mpya - All Rights Reserved
Template Modify by Hisia za Mwananchi
Proudly powered by Hisia