Home » » Shule yaendeshwa bila madawati kwa miaka 40, ipo mkoani SIMIYU.....Wanafunzi wakaa kwenye mawe...

Shule yaendeshwa bila madawati kwa miaka 40, ipo mkoani SIMIYU.....Wanafunzi wakaa kwenye mawe...

Kwa wengi taarifa za ukosefu wa madawati kwenye shule za umma na haswa zile za msingi, siyo za kushangaza. Tumezoea kusikia shule ikiwa na upungufu wa madawati kadhaa lakini siyo kutokuwa na dawati kabisa kwa miaka takribani 40.
Shule ya Msingi ya
Mwaswale iliyopo Tarafa ya Bumela Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, ina historia ndefu ya ukosefu wa madawati kwa kipindi cha miaka 40 sasa.
Tatizo hilo limekuwa ni kero ya muda mrefu hali inayowafanya wanafunzi na walimu wake kukata tamaa ya kuendelea na masomo katika shule hiyo.
Mwaswale ina wanafunzi 1,268 ambao wanalazimika kuketi kwenye mawe kwa sababu ya ukosefu wa madawati.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1973 ikiwa madawati 80, baada ya muda mfupi yaliharibika na kuifanya kubaki kama makumbusho kutokana na wanafunzi wake kukalia mawe au matofali.
Mwandishi wa makala hii alipofika shuleni hapo, alishuhudia wakiwa wameketi kwenye mawe na matofali yaliyopangwa katika mstari na kuleta mtiririko.
Baadhi ya wanafunzi wanasema hali hiyo inatokana na wazazi wao kutoshiriki kuchangia maendeleo ya elimu huku wengine wakiilaumu serikali kwa kushindwa kufuatilia hiyo.
Steven Kwabi anasema licha ya familia nyingi kujihusisha na kilimo wilayani humo, wazazi hawana mwamko katika suala la maendeleo ya elimu.
Mwanafunzi huyo anaiomba serikali na wadau wengine kuwasaidia kupata madawati hali itakayowasaidia kuwaepusha na magonjwa yatokanayo na vumbi.
“Tukipata madawati tutaepuka magonjwa kama mafua na hata kifua kikuu, pia itatusaidia kuandika vizuri tofauti na sasa tunavyoandikia kwenye magoti,” aliongeza.
“Wazazi hawataki hata kuchangia Sh100 za huduma ya uji kwa miezi sita, akiulizwa anasema mbona shule ya jirani hawanywi uji,” anasema Kwabi.
Naye Mabula Masunga anayesoma darasa la tano shuleni hapo, atajisikia vizuri kama shule yake itasaidiwa madawati ili nao wasome kwa furaha kama watoto wa shule nyingine.
“Hapa unaanza darasa la kwanza mpaka la saba hujawahi kukalia dawati, wakati shule kama za mjini kukalia dawati ni kitu cha kawaida,” anasema Masunga.
Anasema kutokuwa na madawati katika shule hiyo, kunasababisha mahudhurio ya wanafunzi kuwa mabaya.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo ya Mwaswale, Mabeja Masanja anasema wanafunzi wa kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba wanaketi chini.
Masanja anasema mbali na tatizo la madawati, huduma ya chakula cha mchana pia hakuna kutokana na wazazi kukataa kuchangia.
Anasema hali hiyo imesababisha kushuka kwa kiwango cha elimu ambapo kwa mwaka juzi wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza, walikuwa ni watatu kati ya 36 waliohitimu darasa la saba.
“Mwaka juzi wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza walikuwa 27 kati ya 121 waliofanya mtihani wa darasa la saba, wasichana waliofaulu walikuwa ni wawili tu,”anasema.
Anasema kuwa, changamoto iliyopo katika shule hiyo ni wazazi kushindwa kutoa chango mbalimbali ya kuchangia maendeleo ya elimu kama vile huduma ya chakula kwa wanafunzi na madawati.
Anasema pia kuwa, imani potofu ni miongoni mwa sababu zinazochangia shule ya Mwaswale ishindwe kutoa huduma ya chakula kwa kile alichosema baadhi ya wazazi huwazuia watoto kula chakula shuleni kwa kuogopa kulogwa.
Mwalimu Mkuu Msaidizi, Emmanuel Charles anasema shule hiyo yenye walimu 14, ndiyo yenye idadi kubwa ya watumishi hao kuliko nyingine zote za Wilaya ya Itilima.
Anasema shule hiyo yenye vyumba tisa vya madarasa, ina upungufu wa madawati 400, ikiwa ni uwiano wa dawati moja kwa wanafunzi watatu. Anaeleza pia kuwa, wana matundu manne ya vyoo lakini mahitaji halisi ni matundu 49.
Viongozi wa elimu wanazungumzia suala hilo.
Mratibu wa Elimu ya Msingi na Sekondari Kata ya Mwaswale, Kidamli Sanangu baadhi ya wanasiasa wakishirikiana na wenyeviti wa kamati za shule, wanamekuwa ni kikwazo cha elimu katika eneo hilo kwenda mbele.
Anasema miongoni mwa wanasiasa hao ni baadhi ya madiwani na wenyeviti wa kamati za shule katika kata za Mwaswale na Sagata zilizopo Tarafa ya Bumela.
Sanangu anasema mwaka 2006 shule hiyo ilipata madawati 200 kupitia mpango wa maendeleo ya elimu shule za msingi lakini madawati hayo yaliharibika mwaka uliofuata kwa sababu hayakuwa na ubora.
Bila kufafanua ni chama gani, Sanangu anasema kuna viongozi wengine wanadai wazazi wakichangia chakula shuleni, walimu watajinufaisha wenyewe .
Anasema mbali na kuwakataza wazazi katika kuchangia huduma ya uji shuleni, viongozi hao huwakataza wazazi kushiriki maendeleo ya shule ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa pindi wanapofanya vikao na wazazi Mratibu huyo anatolea mfano shule ya msingi ya Bumela ambayo ilichimba msingi kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa, ujenzi ulishindwa kutekelezwa kutokana na wazazi kukatazwa na viongozi kutoa michango.
“Ujenzi huo ulikuwa wa madarasa manne na ulitarajiwa kuanza mwaka juzi lakini mpaka sasa hakuna kilichoendelea,” anasema Sanangu.
Baadhi ya wazazi wanasema hali hiyo imesababisha watoto wao washindwe kufanya vizuri katika shule hizo hasa shule ya Bumela yenye wanafunzi 1022 ambayo ina vyumba vya madarasa sita na kufanya kila chumba kuchukua watoto 120 badala ya watoto 45.
Mmoja wa wazazi hao Mwanamabula Maiko anasema hali hiyo inatokana na wivu kati ya viongozi walipo madarakani katika kata hizo na wale ambao hawakufanikiwa kuwa madarakani na hivyo kila mmoja kutoa maagizo kwa upande wake.
Mikakati ya wilaya hiyo
Ofisa Elimu ya Msingi katika Halmashauri ya Bariadi ambaye pia anashughulikia wilaya mpya ya Itilima, Palemon Ndarugiliye anasema mikakati iliyopo kwa sasa ni kuhakikisha kila shule inatoa huduma ya chakula ili watoto wafaulu vizuri mitihani yao.
Ndarugiliye anasema changamoto ni nyingi katika kuchangia maendeleo lakini ni wakati kwa wanasiasa kuhamasisha jamii katika kuchangia maendeleo ya elimu na lishe kwa watoto.
“Tumeandaa kamati zitakazokuwa zinasimamia utoaji wa huduma ya chakula katika shule sanjari na kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa kuchangia maendeleo ya elimu ya watoto wao,”anasema Ndarugiliye.

source: mwananchi
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan Tanzania Mpya untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Hisia za Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Copyright © 2013. Tanzania Mpya - All Rights Reserved
Template Modify by Hisia za Mwananchi
Proudly powered by Hisia