Home » » MSD yapata suluhisho la DAWA BANDIA

MSD yapata suluhisho la DAWA BANDIA

Dar es Salaam. Miezi 10 baada ya kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya kwa tuhuma za kusambazwa kwa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s), uongozi wa bohari hiyo jana umeibuka na kusema kuwa umejipanga kuhakikisha ununuzi wa dawa bandia hautokei tena.
Mbali na kueleza mipango na utendaji wake, bohari hiyo imekiri wazi kuwa, mahitaji ya dawa nchini ni makubwa ikilinganishwa na bajeti inayotolewa na Serikali, kwamba mwaka jana ilihitajika Sh189 bilioni za kununua dawa lakini zilipatikana chini ya Sh100 bilioni.
Imesema tatizo hilo linachangiwa na bajeti finyu, pamoja na uhaba wa viwanda vya kuzalisha dawa nchini, huku ikieleza kuwa kwa sasa kuna viwanda vitatu tu vinavyozalisha dawa nchini. Vingine vikiwa vimefungwa ama kuzalisha dawa za kutibu magonjwa ya aina moja tu.
Akizungumza na Mwananchi mara baada ya kumalizika kwa mkutano wake na wanahabari jana kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Kaimu Mkurugenzi wa Bohari hiyo, Isaya Mzoro alisema hivi sasa wamekiimarisha Kitengo cha Usimamizi wa Ubora wa dawa na kwamba kinafanya kazi zake vizuri, kwa ukaribu mkubwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
“Tumekuwa na mikutano kati yetu na TFDA ili kuhakikisha kwamba tunadhibiti ubora wa dawa zinazowafikia Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa kwa nini bohari hiyo ilinunua dawa bandia ambazo hazikuwa na ubora unaotakiwa alisema, “Hilo suala sitapenda kulisema hapa kwa sababu linashughulikiwa na vyombo vya sheria, usalama wa taifa na polisi, ila kwa sasa kitengo cha usimamizi na ubora wa dawa kimeimarishwa.”
Oktoba mwaka jana Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, alimsimamisha kaz
i Mgaya pamoja na maofisa wengine wawili akiwamo Mkuu wa Kitengo na Ofisa wa Idara ya Udhibiti Ubora, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kusambazwa ARV bandia.
Uamuzi huo ulikwenda sambamba na kufungwa kwa kiwanda kilichotengeneza dawa hizo cha TPI, baada ya kubainika kwa dawa bandia wilayani Tarime.
Dawa hiyo bandia aina ya TT-VIR 30 toleo namba OC.01.85, nyaraka zake zilionyesha kuwa kiwanda cha TPI waliwauzia MSD dawa hiyo iliyotengenezwa Machi, 2011 na kutarajia kwisha muda wa matumizi yake Februari, 2013.
Mzoro alisema mahitaji ya dawa ni makubwa kuliko bajeti ya Serikali na kufafanua kuwa hiyo ndiyo sababu ya maeneo mengine ya nchi kukosa dawa.
“Kwa mfano mwaka jana tulihitaji Sh189 bilioni lakini tulipata fedha chini ya Sh100 bilioni, mwaka huu tunahitaji zaidi ya Sh100 bilioni lakini mpaka sasa fedha tulizonazo ni nusu ya kiwango hicho,” alisema.
Alisema tatizo jingine ni kuwa na viwanda vichache vya kuzalisha dawa nchini na kwamba vilivyopo sasa ni kiwanda cha Shellys, Zenufa na Keko na kwamba viwanda vya Intercane, Tanzasino, TPI na Mansurdaya, ama vimekufa au vinazalisha dawa kwa kiwango kidogo.

Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan Tanzania Mpya untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Hisia za Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Support : Copyright © 2013. Tanzania Mpya - All Rights Reserved
Template Modify by Hisia za Mwananchi
Proudly powered by Hisia