Dar es Salaam. Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele amesema ili kupambana na uingizwaji na uuzwaji holela wa tindikali nchini, waagizaji na wasambazaji wa kemikali aina ya ‘Sulfuric Acid’ wanatakiwa kufuata sheria zilizopo, huku akiwataka wauzaji ambao hawajasajiliwa kuhakikisha wamejisajili katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Wakati Profesa Manyele akieleza hayo, watu wa kada mbalimbali waliliambia gazeti hili kwamba tindikali sasa inapatikana kirahisi, kwamba mtu yeyote akiitaka anaipata.
Walisema watengenezaji wengi wa sabuni, hasa wale waliopo katika viwanda vidogovidogo wana tindikali na wakati mwingine wanazigawa kwa watu bila kujua madhara yake, “Wapo kinamama ninaowafahamu ambao wameungua mikono bila kujua kuwa wanatumia tindikali wakati wakitengeneza sabuni, pia wengine wanauziwa.”
Wasomi wanena
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kuwa jamii inapaswa kujiuliza kwa nini aina hii ya uhalifu imeanza hivi karibuni na kwamba vyombo vya usalama vinatakiwa kuondoa hofu iliyoanza kuwakumba wananchi kutokana na kutapakaa kwa tindikali mitaani.
“Huu ni uhalifu mpya lakini mimi ninaufananisha na mauaji ya albino, ubakaji na unyanyasaji wa watoto na dawa za kulevya. Kwa nini vyombo vya usalama havijaweza kuuzima uhalifu huu?” alihoji Ally.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo-Bisimba alisema vitendo vya kumwagiwa tindikali vinashtua nchi na kwamba wahusika walianza kwa kujaribu waone vyombo vya usalama vitachukua hatua gani.
“Watu wanajaribu waone kitatokea nini, vyombo vya usalama vitafute njia mpya ya kukabiliana na jambo hili,” alisema Kijo-Bisimba.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa wanunuaji wa kemikali hizo hawajui namna ya kuzihifadhi kemikali hiyo wanapofika majumbani mwao, jambo ambalo limechangia baadhi ya ndugu na wanafamilia wa watu hao kudhurika ikiwa ni pamoja na kuungua mikono. “Panga siku uje nikuonyeshe eneo lenyewe ambalo ukitaka tindikali unapata, hali siyo nzuri kabisa ndiyo maana matukio ya watu kumwagiwa tindikali yameongezeka,” kilieleza chanzo hicho.
Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari ambao pia uliwahusisha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Eliezer Feleshi, Profesa Manyele alisema, “Mwanzo tulikuwa tukifanya ukaguzi chini ya ofisi ya mkemia wa serikali kwa ushirikiano na polisi, ila kwa zoezi hili la udhibiti wa tindikali tuliloanzisha sasa ushirikiano lazima uimarishwe ili kupata mrejesho utakaosaidia udhibiti wa makosa ya jinai.”
Alisema wamekuwa wakishirikiana na taasisi nyingine katika kutoa leseni kwa watumiaji halali wa kemikali chini ya sheria hiyo yeyote anayetumia kemikali lazima asajiliwe na ofisi yake na kusisitiza, “Wauzaji wote wa rejareja hawataruhusiwa kumuuzia mteja kemikali, bali wateja watalipia huduma watakayopewa na wauzaji wa rejareja.”
Alisema tindikali hiyo hutumika katika viwanda, hospitali na maabara mbalimbali pamoja na katika usafirishaji (magari). Kauli hiyo imekuja zikiwa zimepita siku tano tangu raia wawili wa Uingereza kumwagiwa tindikali visiwani Zanzibar, tukio ambalo linafanana na matukio mengine yaliyotokea hivi karibuni nchini ya watu kumwagiwa tindikali.
Katika ufafanuzi wake Profesa Manyele alisema watumiaji wote wa kemikali hiyo wanatakiwa kutoa mrejesho kwa mkemia mkuu kila mwezi.
0 comments:
Post a Comment