KUTOKA: GAZETI LA RAIA MWEMA
RAIS Jakaya Kikwete kwa siku kadhaa wiki hii, amekuwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera, ambako amezindua na kukagua shughuli mbalimbali, ikiwamo miradi ya maendeleo. Ni jambo jema kwa Rais kutembelea wapiga kura wake popote nchini, na hasa kama ziara husika imejikita katika shughuli za maendeleo.
Hata hivyo, kwa upande wetu tumesikitishwa na Rais Kikwete kuendeleza mwenendo wake wa kuwa kiongozi wa kuonya zaidi kuliko kuchukua hatua. Rais Kikwete amekuwa akionya tangu ameingia madarakani hadi sasa akielekea kuondoka.
Kimsingi, ukipima kati ya matamko ya Kikwete aliyopata kuyatoa utabaini amekuwa akitoa matamko ya kuonya zaidi hata pasipostahili. Ameonya wazembe serikalini, wala rushwa, wauza dawa za kulevya na hata mafisadi, wakiwamo wa EPA.
Akiwa mkoani Kagera, Rais alizungumzia kuhusu wahamiaji haramu akisema si wavamizi bali wanakaribishwa na kupewa vibali haramu vya kuishi na maofisa wa serikali, bila kujali maofisa hao wako chini ya serikali ya wilaya na mkoa, ambako yeye ndiye aliyewateua wakuu wa wilaya na mikoa.
Kikwete akiwa wilayani Karagwe, Kijiji cha Nyakayanja, Nyaishozi, alisema ni vizuri wahamiaji haramu wakajiondoa na kurudi kwao mapema.
Akasema; “Hili litakuwa jambo zuri kwa sababu sisi (Tanzania) hatutaki wahamiaji haramu watugombanishe na jirani zetu.”
Tumesikita kusikia Rais Kikwete akiungana na wanavijiji kulalamika, na kisha akishauri katika mwelekeo wa kukata tamaa au kuomba msaada kwa wahalifu wawe na huruma, wajisikie kuondoka ili vijiji visiwe na wahamiaji haramu.
Mwenedo huu unanyong’onyesha mno Watanzania wazalendo ambao hawapendi kusikia Rais wao akiomba huruma za wahalifu ili tu mambo yaende vizuri.
Ni dhahiri, mwenendo huu wa Rais unachosha. Tulitarajia afike kwa wanavijiji Nyaishozi na kwingine mkoani Kagera, akijivunia namna maagizo yake yalivyotekelezwa katika kukabili wahamiaji haramu na si kulalamika kama wanavijiji au kutoa maagizo kama tatizo husika hilo ni jipya, limetokea siku moja au mbili zilizopita.
Inashangaza kusikia Rais anawataka wahamiaji haramu waondoke wenyewe kwa hiari, bila kujali anawazungumzia wakiukaji wa sheria za nchi na hata Katiba ya nchi ambayo ameapa kuilinda, ni kama vile anavumilia wahamiaji hao wachezee mipaka ya nchi. Kwa mwenendo huu, Rais Kikwete anachosha wengi.
0 comments:
Post a Comment