Dar es Salaam. Msako wa wezi wa kwenye Mashine za Kutolea Fedha (ATM), umeanza kuzaa matunda baada ya raia wa Bulgaria kukamatwa akiiba kwenye ATM ya Bank of Africa (BOA), Tawi la Afrikana, Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za benki, mtuhumiwa huyo ambaye hakutajwa jina lake alikamatwa baada ya kamera maalumu zilizowekwa kwenye ATM za BOA, kumtambua kuwa ni mwizi sugu wa benki hiyo anayetafutwa.
Mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 12 asubuhi baada ya mtuhumiwa huyo kuwekewa mitambo maalumu ya kumnasa.
Alisema benki hiyo ilipelekewa malalamiko na baadhi ya wateja kwamba wakienda kutoa fedha kwenye ATM wanakuta akaunti zao hazina salio wakati wanaamini zilikuwa na fedha.
Chanzo hicho cha habari kilidai kuwa baada ya kupelekewa malalamiko hayo, waliweka mitambo maalumu ya kuwawezesha walinzi wa maeneo ya ATM za BOA kumbaini mtu atakayetoa fedha kwa njia ya wizi.
“Kama Benki tuliweka mtambo maalumu na mtuhumiwa huyo alionekana kwenye mtambo wetu, hivyo tuliwaagiza walinzi wetu watakapomwona mtu huyo wamkamate haraka sana,”alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alianza mchezo huo kwa muda mrefu ambapo kwa kutumia kadi za ATM zisizojulikana idadi yake, alikuwa anakwenda kwenye ATM mbalimbali za benki hiyo na kutoa fedha hadi Sh10 milioni.
Kuhusu tukio la jana, mmoja wa walinzi wa BOA aliyejitambulisha kwa jina moja la Frenky alisema mtuhumiwa huyo alipofika kwenye ATM hiyo aliingia na kuchukua fedha ambazo alizipeleka kwenye gari lake. Frenky alisema baada ya kupeleka fedha hizo, alirudi kwa mara ya pili ili achukue fedha nyingine ndipo walinzi hao walimkamata na kumfunga pingu.
“Huyu mtuhumiwa mwenye asili ya Kiarabu alifika na gari lake saa 12 asubuhi, aliingia kwenye ATM na kutoa fedha ambazo hazikujulikana ni shilingi ngapi na kuzipeleka kwenye gari lake, baadaye alirejea tena kwa ajili ya kutoa fedha zingine, wakati ana
ingia ndipo alipokamatwa na mlinzi aliyekuwa analinda hapo,” alisema Frenky.
ingia ndipo alipokamatwa na mlinzi aliyekuwa analinda hapo,” alisema Frenky.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, Camilius Wambura alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea.
“Ni kweli taarifa nimezipata, mtuhumiwa amekamatwa, bado hatujajua ni kiasi gani ambacho ameiba kwa kutumia mtandao, tunaendelea na uchunguzi,” alisema Wambura.
Tukio kama hili lilishawahi kutokea mkoani Mwanza Februari 19 mwaka huu na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa kushirikiana na maofisa ya Benki ya NMB liliwatia mbaroni watu watatu ambao walidaiwa kuiba kiasi cha Sh700 milioni kwa nyakati tofauti.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi, Christopher Fuime alisema watuhumiwa hao walinaswa baada ya kuwekewa mtego na maofisa wa benki na polisi saa 6 usiku wa Februari 19, mwaka huu na mtuhumiwa mmoja alibambwa akichukua fedha kwenye ATM ya NMB kwenye Tawi la PPF Plaza Mwanza.
Vifaa walivyokutwa navyo ni kadi bandia 194 za kuchukulia fedha katika ATM za NMB na kati yake kadi 95 zilikuwa na namba 0225152975 zilizotumia namba ya akaunti ya 2258103695 zenye jina na picha ya mtu anayedaiwa kuwa ni Moley L.P.
Kadi nyingine 99 zilikuwa na namba 0506056317 za akaunti namba 5068000322 zikitumia jina moja la Mnuo Z.E na picha moja.
Mbali na kadi hizo waliweza kunasa kadi 36 za Benki ya DTB ambazo kati yake kadi 18 zilikuwa na jina moja la Kelvini G Gratias na namba 20497883, kadi 12 zilitumika jina la J.Paul zenye akaunti namba 2049783 huku kadi sita zikitumia jina moja la Joseph Donald akaunti namba 2049783.
Kadi nyingine tatu zenye maandishi ya Download list na nyingine ikiwa ni kadi ya Visa ya Benki ya KCB yenye namba 413546040003827 zilitumia jina la Elikana Zacharia.
0 comments:
Post a Comment