Wimbila kuendelea kuuawa kwa tembo na wanyama pori wengine limeendelea kushamiri nchini huku likihusisha askari wa majeshi mbalimbali; na juzi askari wawili wa Jeshi la Polisi walikamatwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh. 850,500,000.
Askari waliokamatwa ni Koplo Senga Idd Nyembo na PC Issa Mtama, wote wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Askari hao ni miongoni mwa watuhumiwa tisa waliokamatwa na meno 70 ya tembo ambayo yanaonyesha kwamba wameua tembo 35.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi Jumapili majira ya saa 4:30 usiku katika kizuizi cha Kauzeni, kilichopo Kata ya Visimbulu, Tarafa ya Chole, wilayani Kisarawe.
Alisema watu hao walikamatwa wakiwa na gari aina ya Toyota Surf yenye namba za usajili T 357 ABK, kwa ushirikiano wa Polisi pamoja na askari wa Maliasili baada ya kulitilia shaka.
Alisema wakati wa ukaguzi kwenye kizuizi hicho, ilibainika kwamba kulikuwa na meno 70 ya tembo yenye thamani ya Sh. milioni 850.
Aliwataja watuhumiwa wengine waliokamatwa na makazi yao kwenye mabano kuwa ni Hamidu Hamad (Tandika/Yombo), Mussa Mohamed Ali (Kinondoni Studio), Prosper Maleto (Tandika Khewa), Amiri Bakari (Mbagala Charambe), Seif Kadro Mdumuka (Vikumbulu-Kisarawe) na Ramadhani Athumani (Chanika).
“Waliokamatwa miongoni mwao wapo askari wa jeshi la Polisi, nimeagiza gari iwafuate ili tuweze kuendelea na uchunguzi zaidi.
Wamekamatwa na meno ya tembo yenye thamani kubwa na inaonekana wameua tembo wengi takribani 35 hivi,” alisema Kamanda Matei. Alisema meno hayo yana uzito wa kilo 305.
Hili ni tukio la pili la ujangili linaloripotiwa katika kipindi kisichozidi wiki moja. Jumanne wiki iliyopita, askari magereza watatu wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, walikamatwa na twiga wawili, pundamilia wawili, swala palapala majike wawili na mbuni wawili wenye thamani ya Sh. 55,543,686.20.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati, Paschal Mrina, alisema watuhumiwa hao walikamatwa majira ya saa 6 mchana, wakiwa na gari la magereza aina ya Toyota Land Cruiser, lenye namba za usajili STK 4394.
Mrina aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mrakibu wa Magereza ASP Kimaro Joseph Sauli, WDR Richard Barick Peter na Koplo Silvester Dionis Bukha.
Katika tukio hilo, watuhumiwa wengine ambao ni raia walikuwa ni Abubakari Ngaula, Hamza Mdachi, Saidi Saidi Iddi na Hosseni Gola wote wanadhaniwa kuwa wakazi wa Kiteto ambao alisema walikutwa na bunduki aina ya SAR ya magereza na rifle moja.
Watuhumiwa wote walikuwa na kibali kilichoombwa na Hassani Omari kilichowaruhusu kuua nyati mmoja na pundamilia wawili, lakini walipofika walikiuka sheria na kuua wanyama ambao hawakuwa wamewaombea na pia hawaruhusiwi kuuawa kama vile twiga na swala palapala majike.
Januari 20, mwaka huu, askari wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), Sajenti, Azizi Athumani Yusufu, alikamatwa akiwa na meno ya tembo, eneo la Kibaoni Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Mtuhumiwa huyo alikuwa dereva wa mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe anayefundisha hapa nchini.
Katika tukio hilo, askari huyo alikutwa na pembe mbili za ndovu na bunduki moja aina ya rifle yenye namba 458.
0 comments:
Post a Comment