JAMANI LULU! UMEANZA EEH!



Elizabeth Michael ‘Lulu’.
KWAKO Elizabeth Michael ‘Lulu’. Leo nimeona nikukumbuke kupitia barua! Natambua uwezo wako mkubwa katika kazi, juhudi zako binafsi ndiyo zimekufikisha hapo ulipo, mataifa mbalimbali sasa wanatambua kuwa kuna mtu anaitwa Lulu, yupo Bongo, muigizaji!.
Sitaki kukurudisha sana nyuma lakini najua unajua kuwa ni jinsi gani kipindi cha nyuma ulikuwa ukipamba vyombo vya habari kwa skendo chafu. Ulipoteza dira ya kimaisha, watu wengi waliokuwa wakikufuatilia kazi zako walianza kukutupa.
Walikupotezea kwa sababu ya matukio ya ulevi, mavazi ya nusu utupu na matukio mengi ya ajabuajabu yaliyofanana na hayo. Sina nia mbaya kukumbusha lakini waswahili wanasema binadamu anajifunza kutokana na makosa. Maishani mwako umekutana na mazito yasiyofanana na umri wako.
Kwenye ulimwengu wa mahaba, ilikuwepo minong’ono mingi juu ya watu wanaotajwa kushiriki mapenzi na wewe, walitajwa vigogo, mastaa na hata wasio mastaa. Sitaki kusema ni kweli au la lakini lisemwalo kama halipo, ujue laja.
Siri ilifichuka kupitia kifo cha yule unayedai alikuwa mwandani wako, marehemu Steven Kanumba.
Mazingira ya kifo chake, umri mdogo uliokuwa nao ilikuwa ni fundisho kubwa maishani mwako. Ulipambana na msalaba wa gereza, ukapambana na mlolongo wa kesi mahakamani hadi pale ulipofanikiwa kutoka kwa dhamana, Januari mwaka jana.
Baada ya kutoka mahabusu, kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja sasa ulikuwa kimya, ulionekana kubadilika kitabia. Yale uliyokuwa ukiyafanya awali, uliyaweka pembeni na zaidi kusimamia mustakabali mzima wa maisha yako, ulikuwa mwema sana aisee!.
Kinachonisikitisha ni kuanza kusikia tena matukio ya ajabu, unaonekana kubadilika. Nimefuatilia tabia zako, naona umeanza kubadilika, umesahau eeeh! Mavazi yako kwa miezi michache iliyopita, nimegundua yanaanza kuchepuka! Mfano mzuri ni kigauni ulichokivaa mwishoni mwa wiki iliyopita katika sherehe yako ya kuzaliwa.
Hakikustiri maungo yako nyeti, kilionesha sehemu kubwa ya matiti yako.
Kama hiyo haitoshi, kupitia mitandao ya kijamii umeanza kushusha matusi mazito bila sababu za msingi, mtu akikukosoa kidogo, unampa maneno machafu ambayo hayaandikiki gazetini. Kama kioo cha jamii, unapaswa kuvumilia mengi.
Nikiwa kwenye kazi zangu za kila siku, huwa nakuwa wa kwanza kupata fununu za mabadiliko ya kila msanii na namna anavyoishi. Nikuonye tu, kuwa makini na mwenendo wako kwani tayari jamii ilishaanza kujenga imani na wewe. Uliaminika na ndiyo maana ukapata bahati ya kuchukuliwa katika kampuni nzuri ikakusimamia kazi zako hadi sasa.
Kwa kuwa tayari nimeanza kupata malalamiko kutoka katika vyanzo vyangu, nikusihi sana mdogo wangu, usirudi ulipotoka. Jenga heshima mpya na jamii ikuamini kutokana na kazi zako na si skendo za ajabuajabu, kwa leo ni hayo tu!
Wasalam.
Ni mimi Anko Erick Evarist.
GPL

HIVI NDIVYO WAZIRI MWAKYEMBE ALIVYOUFUMUA MTANDAO WA MADAWA YA KULEVYA UWANJA WA NDEGE........

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana ameanika majina ya watu saba waliohusika kupitisha mabegi tisa yaliyokuwa na kilo 180 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh8 bilioni, Julai 5 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakiwamo maofisa usalama wanne wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na polisi mmoja.
Alisema mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, lakini siku ya tukio hilo mbwa hao walichelewa na walitumika baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.
“Kwa abiria watatu kuwa na mabegi makubwa tisa yanayofanana si kitu cha kawaida kukwepa jicho la maofisa wa ushuru wa forodha na vyombo vya usalama, sijui walikuwa wapi siku hiyo?” alihoji Mwakyembe.
Juzi waziri huyo aliahidi kuyaweka hadharani majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini, na alitekeleza ahadi hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, kusema kuwa watu hao wamenaswa baada ya mfumo wa kamera (CCTV) za uwanja huo kudaka matukio kadhaa yaliyotokea siku ya tukio hilo, kuanzia saa 9:25 hadi saa 10:30 alfajiri.
Ameagiza wafanyakazi hao wanne pamoja na askari polisi mwenye cheo cha koplo, mbeba mizigo na mfanyabiashara aliyekuwa na wasichana wawili waliokamatwa Afrika Kusini, (ambao hatuwezi kuwataja kutokana na kushindwa kuwapata kujieleza) kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kukamatwa na kuunganishwa na watuhumiwa waliokwenda na mzigo huo Afrika Kusini.
Mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya aina ya ‘Crystal Methamphetamine’, yalipitishwa na wasichana wawili wasanii aliowataja kuwa ni Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward ambao walidakwa siku hiyohiyo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini na tayari wameshafikishwa mahakamani.
Juzi Dk Mwakyembe alifanya ziara JNIA kukagua utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku tatu baada ya ahadi aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki mbili, atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege nchini.
Saa nane baada ya ziara hiyo, Maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wanadaiwa kumkamata Edwin Monyo akiwa na kete 86 za dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi aliyokuwa akiisafirisha kwenda Italia kupitia Zurich.
Mpango ulivyosukwa
Alisema siku ya tukio saa 9:28 kamera hizo za usalama zilimwonyesha mbeba mizigo wa uwanja huo akiwa anazungukazunguka eneo la kuingilia abiria kama mtu ambaye ana ahadi na kukutana na mtu fulani.
“Kamera pia zilimnasa ofisa mwingine wa TAA kwa mara kadhaa akitoka na kuingia ndani ya jengo la abiria huku akizungumza na simu, kitendo ambacho hakiruhusiwi kabisa kwa wafanyakazi wa eneo la ukaguzi wa abiria,” alisema na kuongeza;
“Wakati huohuo, kamera zilikuwa zinamwonyesha askari polisi anayetuhumiwa kuhusika katika mpango huo akiwa anarandaranda eneo la uhakiki wa hati za kusafiria kama vile anasubiri kitu fulani.”


Alisema ilipofika saa 10:15 walionekana Agnes na Melisa wakiwa na mfanyabiashara huyo katika eneo la kuingilia abiria huku wakiwa na mizigo na mabegi tisa yaliyofanana.
Alisema kuwa kamera zilimwonyesha polisi huyo akihangaika kuwasaidia abiria mbalimbali kuweka mizigo yao kwenye mashine ya ukaguzi, kazi ambayo alieleza kuwa haikuwa yake.
“Mbeba mizigo anayetuhumiwa kuwa katika mtandao huo alionekana akiwasaidia vijana hao watatu (Agnes, Melisa na mfanyabiashara) kupeleka mizigo yao kwenye mashine ya ukaguzi na baadaye kuyazungushia mabegi hayo katarasi za nailoni na kuyafikisha kaunta ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini,” alisema.
Alisema kamera hizo zilimnasa ofisa wa TAA akimwondoa katika kiti cha ukaguzi wa mizigo mfanyakazi mwenzake, na kukaa yeye ikiwa ni dakika chache kabla ya mabegi tisa ya vijana hao hayajaingia katika mashine ya ukaguzi.
“Kinyume na taratibu ofisa huyo hakujiandikisha kwenye kitabu cha wakaguzi (Screener’s logbook), saa 10:16 akaanza kupitisha mabegi hayo tisa mpaka saa 10:22. Alipomaliza kupitisha mizigo hiyo kwa dakika sita akamwachia ofisa aliyekuwa katika eneo hilo na kuondoka,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema ofisa huyo baada ya kuondoka katika kiti hicho alizungumza kwa dakika kadhaa na askari polisi anayedaiwa kuwa katika mtandao huo na kurejea tena sehemu aliyokaa ofisa mwenzake wa TAA na kumnong’oneza jambo fulani.
“Baada ya hapo akaelekea ukumbi wa abiria huku akiongea na simu, mambo hayo yote yalifanyika huku kiongozi wa sehemu ya ukaguzi akiwa hapohapo bila kushtuka,” alisisitiza.
Alisema baada ya mizigo hiyo kupita katika mashine ya ukaguzi (baggage screening machine), vijana wale watatu wakahamia na mizigo yao kwenye kaunta ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.
“Mabegi matatu ya kilo 20 kila moja yalipitishwa yakabaki mabegi sita ambayo yalitakiwa yalipiwe malipo ya uzito wa ziada. Kwa taratibu za shirika hilo kila kilo moja inayoongezeka hulipiwa dola 5 (Sh8,000), vijana wale walitakiwa kulipia dola 600, lakini walitozwa dola 94 tu ambazo zinathibitishwa na risiti tuliyonayo,” alisema.
Alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida mfanyabiashara ambaye hakuwa na tiketi ya kusafiri siku hiyo, baadaye alibadili mawazo hapohapo na kuamua kuondoka siku hiyo kwenda Afrika Kusini na kulipia gharama ya dola 60 (Sh96,000) ili kupata tiketi.
“Kutokana na hali hiyo mhakiki wa nyaraka za safari nje ya ukumbi wa abiria siku hiyo, hakupaswa kumruhusu mfanyabiashara kuingia ndani ya ukumbi bila tiketi ya siku hiyo,” alisema na kuongeza;
“Kwa hali ya kawaida mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa, lakini siku hiyo mbwa walichelewa na walikuja kutumika baadaye ikiwa ni baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.”

Hatua za wizara
Alisema wizara imeagiza TAA kuwa, kuanzia sasa mtu yeyote anayekamatwa na dawa za kulevya lazima apigwe picha na zisambazwe kwenye vyombo vya habari.
Pia ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kumkamata mfanyabiashara anayedaiwa kuwasaidia Masogange na mwenzake kusafirisha dawa za kulevya ambaye alitoweka na mabegi matatu ya dawa hizo huko Afrika Kusini, “Akamatwe na kuunganishwa na kesi inayowakabili Watanzania hao wawili.”
Alisema mbeba mizigo anatakiwa kufukuzwa kazi na mwajiri wake na asiruhusiwe kukanyaga JNIA, kwamba serikali imewaagiza polisi kumkamata mtu huyo kwa lengo la kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka ya jinai chini ya sheria ya kuzuia dawa za kulevya, sura ya 95 ya mwaka 1996.
Alisema TAA inatakiwa kuwafukuza kazi mara moja wafanyakazi wake wanne waliohusika katika mpango huo, kuwakamata na kuwaunganisha katika mashtaka yanayowakabili.
“Jeshi la polisi limeagizwa kumwondoa mara moja askari mwenye cheo cha koplo anayedaiwa kuhusika katika tukio hilo na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwa njia moja au nyingine kwenye njama za kupitisha mabegi hayo ya dawa za kulevya,” alisema.
Alifafanua kuwa Idara ya Usalama wa Taifa imeagizwa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu siku ya tukio kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wakati mwafaka, jambo ambalo limeliletea taifa fedheha kubwa.
“Serikali imeziagiza taasisi zote zilizopo chini ya JNIA kutekeleza majukumu ipasavyo na kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kuhakikisha dawa za kulevya hazipiti kwenye kiwanja hicho kikuu cha ndege nchini,” alisisitiza.

BAKWATA sasa yamuunga mkono PONDA, yawaponda POLISI..........

 Baraza la waislamu Tanzania BAKWATA limeitaka serikali kuunda tume huru ya uchunguzi na kumtaka kamanda wa polisi mkoani Morogoro Faustine Shilogile kujiuzulu ili kupisha tume hiyo itakayoundwa kulifanyia uchunguzi madai ya tukio la katibu wa jumuia na taasisi za Kiislamu nchini shekhe Ponda Issa Ponda kupigwa risasi na polisi mkoani humo huku familia yake ikitoa msimamo wao kuhusiana na tukio hilo.
Msimamo huo wa BAKWATA umetolewa na sheikh mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum katika makao makuu ya mkoa ya baraza hilo na kuongeza kuwa licha ya Bakwata kutofautiana kifikra na Sheikh Ponda hawaungi mkono kwa namna yeyote ile tukio hilo la madai ya kupigwa risasi na polisi huku akilitaka jeshi la polisi nchini kujipanga upya katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuepuka matumizi makubwa ya nguvu ikiwa ni pamoja na kutumia risasi za moto kwa raia kwa kuwa hali hiyo inachafua sura na amani ya nchi iliyopo hivi sasa na kuwataka wote waliohusika katika tukio hilo kuwajibishwa.
Sheikh Alhad ameonya kuwa endapo itathibitika pasi na shaka kuwa sheikh Ponda amedhuriwa kwa risasi ya moto na jeshi la polisi ni dhahiri kuwa mahusiano mema baina ya raia hasa wa jamii ya kiislamu na polisi yatakuwa ni ya mashaka.
Akizungumza na vyomba vya habari katika taasisi ya tiba ya mifupa na upasuaji wa mishipa ya fahamu, MOI meneja uhusiano wa MOI Juma Almas amekiri sheikh Ponda kulazwa hospitalini hapo na kwamba imekuwa ni vigumu kujua majeraha aliyo nayo yamesababishwa na kitu gani kwa kuwa majeruhi alifikishwa katika taasisi hiyo akiwa tayari ameshashonwa jeraha.
Katika taasisi ya tiba ya mifupa na upasuaji wa mishipa ya fahamu,moi alikolazwa sheikh ponda issa ponda ambapo itv imemtembelea na kuonana nae licha ya kutozungumza lolote msemaji wa familia hiyo amesema wanapata mashaka kutokana na kile alichokiita kuwa ni upotoshaji wa makusudi unaofanywa kuficha sababu za sheikh Ponda kuumizwa na kusema kile familia inachoamini kimemdhuru sheikh Ponda.
Katika eneo hilo la wodi alikolazwa sheikh Ponda kumeonekana uwepo wa ulinzi mkali ambapo ITV imeshuhudia askari kanzu pamoja na baadhi ya askari waliokuwa na silaha wakilinda eneo lote la wodi hiyo.
 
source ITV TZ

SAKATA LA KUMWONDOA MEYA: CCM hoi Bukoba, Madiwani wapewahongo, watishiwa kufukuzwa uanacham

HATUA ya madiwani wanane wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika manispaa ya Bukoba, kusaini hati ya tuhuma na kuiwasilisha barua hiyo kwa mkurugenzi wa manispaa hiyo, kumtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kutokuwa na imani na meya anayetuhumiwa kujiingiza katika miradi ya kifisadi imechukua sura mpya.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana jioni kutoka mjini Bukoba, zilisema kuwa msimamo huo umewagawa viongozi wa CCM mkoa wa Kagara na hivyo kuitisha kikao cha halmashauri ya mkoa leo kwa ajili ya kuwajadili na kuwafukuza madiwani hao.
Hata hivyo uamuzi huo, huenda ukakigharimu chama hicho kutokana na madiwani hao kusisitiza msimamo wao, wakisema wako tayari kufukuzwa kwa sababu wanatetea maslahi ya wananchi wakipinga ufisadi.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili kwa masharti ya kuhifadhiwa jina lake, mmoja wa madiwani hao alisema kuwa rushwa imekuwa ikitembezwa waziwazi kwa wajumbe wa vikao mbalimbali vya CCM ili kuwalazimisha wakutane mara kwa mara kufikia uamuzi huo.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa katika kuwagawa madiwani hao ambao wameungana na wenzao wa vyama vya CHADEMA na CCM ili kupunguza idadi ya akidi, diwani mmoja alijaribiwa kuhongwa milioni 20 ili aondoe jina lake katika orodha hiyo.
“Mwenzetu mmoja kwa kweli amekuwa jasiri wa ajabu, juzi aliitwa mahala akatumiwa watu wakiwa na fedha taslimu milioni 20 lakini alikwepa mtego huo na kuwakimbia watu waliotumwa, akisisitiza kuwa hawezi kutusaliti. Sasa kwa hali hii kama CCM wanadhani wanaweza kukinusuru chama kwa kutufukuza na wajaribu waone,” alisema.
Naye diwani mwingine alidokeza kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wilaya na mkoa ndio wanatumika kuwarubuni madiwani hao kwa rushwa ili waondoe tuhuma hizo dhidi ya meya, Anatory Amani.
Hivi karibuni, madiwani hao walimgeuka Rais Jakaya Kikwete, wakipinga uamuzi wake wa kumtaka meya kumaliza tofauti zake na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwa kile walichodai mgogoro huo si ugomvi kati ya wawili hao.
Madiwani hao walipinga kauli hiyo wakisema suluhu ni kupinga ufisadi wa meya, kwani hakuna ugomvi binafsi kati yake na mbunge.
Akihutubia mkutano mjini Bukoba, Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo lazima uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano “yasiyokuwa na msingi”.
Madiwani hao 15 walisema malumbano yaliyopo ni ya msingi kwa kuwa watu watakaobebeshwa deni la kurejesha mikopo inayochukuliwa na meya ni wakazi wa Bukoba, si meya mwenyewe.
Walisema Rais ameonekana hafahamu kiini cha mgogoro, kwani kinachopingwa si miradi, bali utaratibu ambao meya ametumia kuanzisha miradi hiyo kifisadi bila kuzingatia maslahi ya wananchi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Barua ya madiwani hao, iliwasilishwa jana asubuhi saa 2.30 na kupokelewa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Shimwela L.E, ikiwa na saini za madiwani 16 kati ya 24 waliopo.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo, alipotafutwa na gazeti hili alishindwa kukiri au kukanusha kupokea barua hiyo, akisingizia kuwa kwa muda huo alikuwa akitekeleza majukumu yake nje ya ofisi.
“Unajua Rais juzi aliacha maagizo mengi na baya zaidi ni lile la ugawaji wa viwanja, hivyo asubuhi niliingia ofisini na kutoka kuelekea mitaani. Nitakupa taarifa kesho kama barua hiyo imefika,” alisema.
Kwa mujibu wa kanuni za manispaa hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM, ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.
Kanuni hizo pia zinaelekeza kuwa mkugenzi atapaswa kuitisha kikao hicho ndani ya siku saba kuanzia tarehe aliyopokea barua ya tuhuma hizo za madiwani na ndani ya muda huo anapaswa kuwa amempatia mtuhumiwa tuhuma hizo ili aweze kuzijibu.
Alisema walikuwa wamesaini madiwani 16 lakini waliamua kumtoa Balozi Kagasheki kwa vile ni waziri na sehemu ya serikali, hivyo walibakia madiwani 15. Hata hivyo, inajulikana kuwa hata Kagasheki anawaunga mkono itakapofika hatua ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.
Madiwan hao wanaompinga meya ni Richard Gaspar (CCM), Rabia Badru (CUF), Murungi Kichwabuta (CCM), Winfrida Mukono (CHADEMA), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (CCM), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Deusdedit Mutakyahwa (CCM), Robert Katunzi (CCM), Samwel Ruhangisa (CCM) na Dauda Kalumuna (CCM).
Wengine ni Dismas Rutagwelela, Israel Mlaki wa CHADEMA na Conchester Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho pamoja na Ibrahim Mabruk, Felician Bigambo wa CUF.

source: Tanzania daima

"MZUNGU" AKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI ZENYE THAMANI YA ZAIDI YA SH.MILIONI 100

RAIA wa Uingereza, Robert Dewar, amekamatwa na nyara za serikali zenye thamani ya sh 118,314,900 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, mtuhumiwa huyo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trans Afrikas Logistics (TALL), akikamatwa Agosti 9, mwaka huu, akiwa na nyara hizo.
Alizitaja nyara hizo kuwa ni vipande vinane vya meno ya tembo, vinyago 11, meno ya tembo 20, meno 20 na kucha 22 za Simba, ndege mmoja aina ya kasuku, vipande vya miti ya mpingo na idadi kubwa ya vinyago, vyote vikiwa na uzito wa kilogramu 24.
Mtuhumiwa huyo pia alikutwa akiwa na mawe yanayodhaniwa kuwa ni madini pamoja na ganda moja la bomu lenye ukubwa wa milimita 130.
Kamishna Kova aliongeza kuwa mtuhumiwa amekuwa akisafirisha vitu hivyo sehemu mbalimbali duniani, na kwamba atafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limeahidi zawadi nono ya sh milioni 100 kwa mtu atakayetoa au kufanikishwa kukamatwa wahalifu wanaotuhumia kutumia tindikali kuwadhuru watu mbalimbali.
Kamishna Kova alisema kuwa matukio hayo yamekithiri nchini, ikiwamo tukio la raia wa Lebanon ambaye ni Mkurugenzi wa Home Shopping Centre jijini Dar es Salaam kumwagiwa kemikali iliyomletea madhara makubwa.
Katika hatua nyingine, watu wawili wamesomewa shitaka katika Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Ilala wakikabiliwa na tuhuma za wizi wa kutumia silaha.
Washtakiwa hao, Abdalla Shamte (30) na Mussa Hassan (40) wanadaiwa kuiba mabati 47 na vipande 11 vya mbao, vyenye thamani ya sh 3,084,000 mali ya Dk. Justine Paul.
Washtakiwa wote walikana kosa hilo lilisomwa na Mwendesha Mashtaka, Munde Hamisi, mbele ya Hakimu Joyce Minde.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 26, mwaka huu na washtakiwa walipelekwa rumande.

source: Tanzania daima

LINDI: Maajabu, mtoto azaliwa na midomo ilyoungana......

Mkazi wa kijiji cha Nyengedi mkoani Lindi, Khadija Hokororo (25),  amejifungua mtoto wa kike huku  midomo yake ikiwa imeungana.
Hali hiyo inamfanya mtoto huyo anyonye kwa shida maziwa na mama yake.

Habari zilizopatikana kijijini hapo zilieleza kuwa mtoto huyo alizaliwa katikazahanati ya kijiji hicho, Agosti 2, mwaka huu majira ya usiku.

NIPASHE lilifika kijijini hapo na kumshuhudia mtoto huyo midomo yake ikiwa imeungana na pua pamoja na matundu mawili sehemu ya mdomo wake.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi pamoja na Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Thomas Ngomo, walisema mtoto huyo alizaliwa katika zahanati ya Nyengedi, iliyopo katika kata hiyo kwa msaada wa muuguzi Elizabeth Raisi.

Aidha, walisema hilo ni tukio la kwanza kutokea kwa mtoto mwenye tatizo kama hilo kuzaliwa kijijini hapo.

Mama wa mtoto huyo, Hadija Rashid, alisema ni kama mkosi kwake ikizingatiwa ni kijana wake wa kwanza mwenye ulemavu kati ya watoto wake wawili.

“Huyu ni mtoto wangu wa pili, lakini huyu wa kwanza siyo kwa mume niliyenaye sasa...Mwenyezi Mungu ameamua kunijalia hivyo siwezi kumfanyia ubaya wowote kama wafanyavyo baadhi ya wanawake wenzangu. Nitamlea kama kawaida kwani yote yametokana na mapenzi yake Mungu,” alisema Khadija.

Alisema kwa sasa anatumia njia nyingine kumnywesha maziwa mtoto wake huyo ikiwamo kuyakamua na kuyaweka katika chombo kisha kummiminia kupitia kwenye matundu mawili yaliyopo eneo ambalo mdomo umeungana.

Mume wa mwanamke huyo, Salum Mnong’one, alisema baada ya kuzaliwa kwa mtoto huyo,  walimpeleka katika hospitali ya Nyangao kwa msaada zaidi.

Hata hivyo, alisema wataalam wamemshauri ampeleke jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Kairuki kwa uchunguzi zaidi.

“Hivi sasa nipo katika kujitafutia nauli nimpeleke akapate tiba itakayomuwezesha mwanangu aweze kunyonya," alisema.

Aidha, muuguzi aliyemsaidia mama wa mtoto huyo kujifungua, Elizabeth, alisema hiyo ni mara yake ya kwanza kuzalisha mtoto akiwa na matatizo ya aina hiyo.

Source: Nipashe

POLISI YAWATIA MBARONI WAUAJI WA BILIONEA WA MADINI ARUSHA

Wakati bilionea mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite yanayopatikana Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, marehemu Erasto Simon Msuya (43) akitarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwao mtaa wa Kairo, Mji mdogo wa Mirerani, polisi imewatia mbaroni watu wawili wakihusishwa katika mtandao uliofanya mauaji ya mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara huyo anayemiliki vitega uchumi kadhaa katika miji hiyo, aliuawa Agosti 8, mwaka huu katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai baada ya kumiminiwa risasi zaidi ya 20 za bunduki ya kivita aina ya SMG.
Habari zilizopatikana jana Arusha, zilidokeza kuwa washukiwa hao walikamatwa siku ya tukio huko Sanyajuu wilayani Siha, kilomita chache kutoka mahali ilipotelekezwa pikipiki iliyotumika katika mauaji hayo.
Pikipiki hiyo mpya ilitelekezwa katika Kijiji cha Olkolili baada ya kupata pancha gurudumu la mbele na watu waliokuwa wakiitumia waliiacha na kuamua kutembea kwa miguu.
Habari zinadai kuwa watu hao wawili sio waliomfyatulia risasi mfanyabiashara huyo bali wana ‘taarifa muhimu’ zinazohusiana na mpango mzima wa mauaji hayo na mtandao wa watuhumiwa waliohusika.
Inadaiwa kuwa baada ya wauaji wa mfanyabiashara huyo kutelekeza pikipiki hiyo, ‘waliwezeshwa’ kutoroka kupitia Wilaya ya Simanjiro na baadaye kuingia jijini hapa ingawa hawajulikani mahali waliko.
“Ni kweli kuna watu wawili walikamatwa na wanashikiliwa kule Makao Makuu ya Polisi Moshi na kila siku wanaletwa hapa Arusha kwa ajili ya uchunguzi wa kuwatafuta wahusika hasa,” alidokeza polisi mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuelezea zaidi baada ya simu yake kutokupatikana.
Ofisa huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema hata hiyo jana, timu ya wapelelezi kutoka Moshi wakiongozwa na RCO Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi walikuwapo jijini hapa na watuhumiwa hao.
Uchunguzi zaidi wa polisi kuhusu mmiliki halali wa pikipiki iliyokuwa ikitumiwa na vijana wawili waliotekeleza mauaji hayo, zimebaini kuwa bado inamilikiwa na kampuni moja ya Dar es Salaam iliyouza pikipiki hiyo.
Habari zaidi zinadai kuwa pikipiki hiyo ilinunuliwa mahususi kwa ajili hiyo na mwanamke mmoja ambaye hafahamiki na ilinunuliwa katika duka ambalo ni tawi la kampuni iliyoingiza pikipiki hiyo lililopo Arusha.
Mfanyabiashara huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa kesho, huko Mirerani, aliuawa baada ya kuitwa kwa simu na wauaji waliojifanya ni vijana wenye madini ya Tanzanite waliotaka kumuuzia marehemu.


Alisema ameacha mke na watoto wanne, wawili wa kike na wawili wa kiume na ameacha rasilimali nyingi zikiwamo nyumba ya kifahari,migodi,hoteli maarufu za SG Resort na Mezza Luna zilizopo Arusha.
Pia, ameacha magari mengi ya kifahari ikiwemo Range Rover Vogue (New Model) ambalo alikuwa nalo wakati akipigwa risasi kwenye eneo la mijohoroni (kwa wasomali) kati ya Boma ng’ombe wilayani Hai na uwanja wa ndege wa Kia.
Hata hivyo, marehemu alipofika eneo hilo akiwa na gari lake la kifahari aina ya Range Rover toleo jipya, alishuka kwenda kuzungumza na vijana hao mita kama 70 kutoka kwenye gari lake na ndipo alipomiminiwa risasi.
Inadaiwa kuwa baada ya vijana hao kumuua, walichukua begi jeusi lililokuwa na fedha ambazo angezitumia kununulia madini hayo lakini hawakuchukua simu wala bastola ya marehemu anayoimiliki kihalali.
Kumekuwapo na taarifa zinazotatanisha kuhusu kiasi hasa kilichoibwa huku taarifa zikidai ni Sh50 milioni na nyingine zikidai ni Sh120 milioni.
Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alikaririwa na gazeti hili akikanusha taarifa kuwa ndani ya gari la marehemu kulikuwapo na kiasi cha fedha Sh150 milioni kilichokutwa.
Mazishi kufanyika kesho
Akizungumza na gazeti hili jana, Shujaa Godfey ambaye ni shemeji wa marehemu Msuya, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (Seliani) na mazishi yatafanyika kesho.
Shujaa alisema mtoto mkubwa wa marehemu, Simon Erasto ambaye anasoma nchini Australia, aliwasili jana Jumapili kwa ndege baada ya kutua Dar es Salaam na kupanda tena ndege iliyomshusha Kia kwa ajili ya kushiriki mazishi kesho.
“Kabla ya kifo chake, marehemu Msuya aliacha wosia kuwa azikwe mtaa wa Kairo na misa ya mazishi yake ifanyike kwenye Kanisa la Lutherani lililopo Kairo ambalo alichangia nguvu kubwa katika kulijenga,” alisema Shujaa.
Kifo cha Msuya kilichotokea Jumatano iliyopita ya Agosti 7 mwaka huu, kwa kuuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20, kiliacha gumzo kwenye miji ya Arusha Moshi na Mji mdogo wa Mirerani ambapo ndipo nyumbani kwao.
Katika mazishi ya kesho, watu mbalimbali maarufu nchini wanatarajia kushiriki wakiwamo wa chama na Serikali, wabunge na viongozi wa vyama vya kisiasa kwani enzi za uhai wake Msuya alikuwa kada maarufu wa CCM.
Shujaa alisema marehemu Msuya alizaliwa mwaka 1970 huko Shighatini wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro na alipata elimu ya msingi shule ya Shighatini mwanzoni mwa miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90 akajiunga na Shule ya Sekondari Makumira iliyopo mji mdogo wa Usa River wilayani Arusha kwa kidato cha nne na kisha akajiunga na Shule ya Sekondari Tanga kwa kidato cha sita.
“Mwishoni mwa miaka ya 90 alichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu Dar es salaam kusomea Shahada ya Uchumi ila aliacha kwenda na akawa anajishuhulisha na uchimbaji na ununuzi wa madini,” alisema Shujaa.

Hatimaye PONDA aingia mikononi mwa polisi, Alazwa MOI, Polisi yakanusha kumpiga risasi, yaweka ulinzi mkali MUHIMBILI

Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake Dar es Salaam kuwa chama hicho kinalaani vikali tukio hilo na kutaka polisi kuwakamata waliompiga risasi.
“Nimetoka kumjulia hali muda mfupi uliopita, nimemkuta akiwa katika hali mbaya japo anaweza kuzungumza na kutambua watu wanaokwenda kumwona... kwa kweli tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda linaweza kusababisha nchi kuingia kwenye machafuko ya kidini kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Tukio la Sheikh Ponda kupigwa risasi tena na watu wanaodhaniwa kuwa ni polisi, limeleta sura mbaya kwa taifa,” alisema Lipumba.
Rufaa ya wafuasi wake leo
Wakati hayo yakitokea, rufaa ya wafuasi 52 wa Sheikh Ponda waliohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Wafuasi hao walihukumiwa kifungo hicho, Machi 21, mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, kutenda makosa, kukaidi amri ya polisi kabla na baada ya kufanya maandamano yaliyozuiwa na polisi, kufanya mikusanyiko haramu na kusababisha uvunjifu wa amani na uchochezi.
Hata hivyo, kupitia kwa Wakili wao,
Mohamed Tibanyendera walikata rufaa wakipinga hukumu na adhabu waliyopewa.
Rufaa hiyo itasikilizwa leo na Jaji Salvatory Bongole.
Kwa mujibu wa hati ya rufani waliyoiwasilisha mahakamani hapo, wafuasi hao, pamoja na mambo mengine, wanadai kuwa hakimu alikosea kisheria katika kuchambua ushahidi wa pande zote uliowasilishwa mahakamani.
Pia wanadai kuwa katika hukumu hiyo, hakimu alijikanganya kwa kumwachia huru mmoja wa washtakiwa na kuwatia hatiani washtakiwa wengine.
Watu hao walikamatwa na Polisi Machi 15, mwaka huu, wakiandamana kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa lengo la kumshinikiza kumpa dhamana Sheikh Ponda na mshtakiwa mwenzake Mukadam Swalehe na Machi 18, mwaka huu walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka.

Hisia za Mwananchi T-Shirt, Kupatikana hivi karibuni kwa bei ya Tsh. 10,000/= tu, Kaa tayari

FAIDA KUBWA YA KABICHI~~~(Kinga kubwa dhidi ya saratani):

NYUMBA YA UKAHABA LAGUNDULIKA DAR: Lipo kama guest, hutumika kama danguro la kuuzia miili na wanawake

JUMBA linalodaiwa kutumika kuendesha shughuli za ukahaba limebainika kuwapo katika eneo la Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili, umebaini kuwapo kwa jumba ambalo linatumika kama nyumba ya kulala wageni, ambako idadi kubwa ya makahaba hujazana na kuendesha biashara ya kuuza miili yao bila wasiwasi.
Imebainika kuwa, wasichana wanaofanya biashara hizo hutoza kiasi cha sh 5,000 kama huduma ya ngono na chumba kwa matumizi ya muda mfupi.
Biashara hiyo ambayo im
eleta usumbufu mkubwa kwa wakazi wengi wanaopakana na nyumba hiyo, imekuwa ikifanikiwa kutokana na kuwapo kwa baadhi ya askari polisi wanaodaiwa kuwalinda wasichana hao pamoja na mmiliki wa nyumba hiyo.
Nyumba hiyo inavyo vyumba vingi vinavyotozwa kiasi sha sh 1,200 kwa chumba pamoja na kondomu. Kadhalika wasichana wenye umri wa miaka 15, ni miongoni mwa wanaofanya biashara hiyo.
Mjumbe wa serikali ya mtaa wa eneo hilo, Amiri Banza, alikiri kuwapo kwa biashara hiyo, ingawa alisema wamejaribu sana kuzuia hali hiyo bila mafanikio.
“Tumechoka na hii kadhia, tumeripoti kwa viongozi wa kata hadi polisi lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, kama wakija polisi wanawakamata halafu wanawaachia,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi alipoulizwa juu ya kuwapo kwa jumba hilo alisema hajui chochote.
“Mimi sijapata taarifa hizo na ndiyo kwanza ninakusikia wewe,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu polisi kufika kwenye jumba hilo na kuchukua rushwa na kuondoka alisema: “Sina ushahidi, kama wapo polisi wanafanya hivyo ni kosa,” alisema Minangi na kuongeza kuwa polisi wanafanya doria maeneo hayo na mara kadhaa wamewakamata watu wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwafikisha mahakamani.

From: Tanzania daima

SAKATA LA KUTEKWA KWA ULIMBOKA: Serikali sasa yamlaumu ULIMBOKA kwa kuficha ushahidi

SIKU chache baada ya Mahakama ya Kisutu kumwachia mtu aliyedaiwa kumteka na kumtesa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, serikali imemshukia daktari huyo na kudai ndiye chanzo cha kukwama kwa dola kukamata watu waliomteka.
Jana Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Eliazer Feleshi, alidai kuwa vyombo vya dola vimeshindwa hadi sasa kuwakamata waliohusika katika shambulio hilo kutokana na Dk. Ulimboka kukwepa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

Feleshi ambaye jana aliambatana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alidai lawama zinazosukumwa kwa Jeshi la Polisi kwa madai ya kushindwa kuwakamata waliomtendea unyama daktari huyo hazina msingi, kwa kuwa mhusika mwenyewe hajafika polisi, licha ya kuitwa mara nyingi kutoa maelezo.
Alisema kama Dk. Ulimboka angetoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kungekuwa na mafanikio makubwa katika kuwasaka na hata kuwatia mbaroni waliohusika katika unyama huo.
“Kila mara mmekuwa mkilaumu polisi wanashindwa kukamata wahalifu lakini tutakamataje kama wenye ushahidi hawataki kutoa ushirikiano?
Kwa mfano mdogo tu ni ‘ishu’ (suala) ya Dk. Ulimboka, hadi leo hajatoa taarifa lakini polisi wanaendelea kusakamwa na kutukanwa tu,” alisema.
Hata hivyo, wakati Feleshi akitoa kauli hiyo, Dk. Ulimboka katika andiko lake alilolitoa mara tu baada ya kurejea nchini kutoka Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu, alimtaja mtu anayeaminika kuwa mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye aliyemteka na kumtesa.
Ulimboka akimtumia Wakili Nyaronyo Kicheere alisema Ighondu na wenzake ni mhusika mkuu katika unyama aliofanyiwa, kauli ambayo imekanushwa mara kadhaa na serikali.
Mapema wiki hii, raia wa Kenya, Joshua Mulundi, aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka aliachiwa na Mahakama ya Kisutu baada ya DPP Feleshi kumfutia shitaka. Hata hivyo Mulundi alikamatwa tena na sasa amefunguliwa mashitaka ya kutoa maelezo ya uongo kwa polisi.
Wakati DPP akisema hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, jana aligoma kuzungumzia shinikizo la kumtaka ajiuzulu kutokana na kukithiri kwa matukio ya raia kumwagiwa tindikali, badala yake amewataka Watanzania kuwa na ushirikiano wa pamoja kukabiliana na uhalifu huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, (IGP) Mwema alishindwa kukubali kujiuzulu wadhifa huo na badala yake alitoa majibu ya jumla huku akiwataka Watanzania kubadilika na kuona suala la kulinda raia na mali zao ni jukumu la kila mmoja na si kazi ya polisi pekee.
Mkuu huyo alisema kuwa Watanzania lazima waelewe kuwa suala la ustawi wa jamii linatokana na uwepo wa amani na utulivu. “Nchi hii si ya mtu mmoja bali ni ya kila Mtanzania, inashangaza kuona asilimia 89 ya Watanzania wanaona suala la kulinda raia ni la polisi, si kweli ni lazima tubadilike,” alisema.
Alisema kuwa jukumu la utu lipo pale pale, hivyo kama taifa wana dhamana ya kuhakikisha suala la matumizi mabaya ya tindikali na dawa za kulevya linakomeshwa.
Mwema alisema kuwa wanalaani vitendo vibaya na vya kikatili vinavyofanywa na mtu mmoja mmoja ambavyo vinaleta hofu kwa jamii.
Alisema kuwa juhudi mbalimbali zinafanywa kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa na hata kumalizwa kabisa. “Tumeamua kuja na mkakati wa pamoja kwa kuwa sasa matukio ya umwagiaji tindikali umeshamiri na hatuwezi kusubiri adhurike mtu mwingine, bali tusaidiane wote kwa pamoja kukomesha haya,” alisema.
Alisema kuwa lengo la kutengenezwa kemikali hiyo haikuwa kutumika vibaya au kumdhuru binadamu, bali ni muhimu kwa ajili ya vyombo vya usafiri na maabara.
“Hata kisu ukiangalia kimetengenezwa kwa ajili ya mambo ya msingi, lakini kikitumika vibaya kinaweza kudhuru watu,” alisema.
Huku akionyesha hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo bila kutaja jina, alisema kuwa ofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mmoja amesimamishwa kazi baada ya kudaiwa kuruhusu kupita kwa mabegi tisa ya dawa za kulevya yaliyokamatwa Afrika Kusini mwezi uliopita.
Mwema alisema kuwa ni muhimu wananchi wakatoa taarifa mapema pindi waonapo mwenendo mbaya wa matumizi ya tindikali hiyo, kwa kuwa ni uhalifu mpya.
“Wananchi ndio waathirika wa kwanza, ni vema wakatoa taarifa mapema ili hatua ziweze kuchukuliwa, maana vyombo vya dola pekee haviwezi kuhimili jambo hilo,” alisema.
Matukio ya kumwagiwa tindikali kwa sasa yameshamiri nchini kufuatia baadhi ya raia kupata ulemavu na wengine vifo, huku Julai 19, mwaka huu mmiliki na mfanyabiashara maarufu wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad, akivamiwa na kumwagiwa maji usoni yanayodhaniwa kuwa ni tindikali.
Ikiwa ni takriban wiki mbili tangu kutokea kwa tukio hilo, juzi wasichana wawili raia wa Uingereza waliofika visiwani Zanzibar kujitolea kufundisha somo la Kiingereza walimwagiwa tindikali majira ya saa 1:15 usiku, Mtaa wa Shangani eneo la mji Mkongwe.
Hata hivyo wasichana hao walisafirishwa jana kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mwaka 2007 Mkurugenzi wa Halihalisi Publishers, Said Kubenea, alimwagiwa tindikali, hatua inayomlazimu kwenda nchini India mara kwa mara kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Mwaka 2011 wakati wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Igunga, Musa Tesha, alimwagiwa tindikali, huku mkoani Arusha, wilayani Arumeru, Sheikh wa wilaya hiyo, Said Juma Makamba, alijeruhiwa kwa kumwagiwa usoni kimiminika kinachoaminika kuwa tindikali.
Wakati Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, Novemba mwaka jana alimwagiwa tindikali.
Mkemia Mkuu wa Serikali
Katika kikao cha jana, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyere, alipiga marufuku usafirishaji wa tindikali bila kibali na kuagiza wahusika kutunza kumbukumbu kuonyesha ukali wa tindikali na kutoa mrejesho wa kiasi walichouza kuanzia mwezi huu.
Alisema kuwa wasafirishaji wanapaswa kuwa na vibali kisheria ambavyo vimetolewa na ofisi yake.
Profesa Manyere alisema kuwa wauzaji wa rejareja ni lazima wawe wamesajiliwa na wanapaswa kutoa taarifa za mauzo wanayofanya kila baada ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Alisema kuwa kuanzia sasa wamiliki wa vyombo vya usafiri hawaruhusiwi kuchukua kemikali hiyo na kwenda nayo nyumbani badala yake wapeleke magari yao. “Wale wa lita moja moja hawaruhusiwi kuuziwa bali itapaswa kuuzwa kuanzia lita tano na kuendelea,” alisema.

from: nipashe

NIMRODI MKONO naye apinga serikali tatu, adai kuwa, una lengo la kutugawa kama kipindi cha ukoloni

Mjadala unaoendelea kuhusu rasimu ya Katiba Mpya, unayagusa makundi mengi ya kijamii na watu binafsi, kila upande kwa namna yake.
Lakini sehemu kubwa ya mjadala huo imejikita katika muundo wa utawala wa nchi, ambapo rasimu hiyo iliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Katiba, imependekeza kuwapo serikali tatu. Pendekezo hilo, limechukua sehemu kubwa katika mjadala unaoihusu rasimu hiyo.
Mmoja wa watu ni Nimrodi Mkono, Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM) na mwanasheria aliyebobea katika tasnia hiyo kwa miongo kadhaa sasa.
Mkono, anajenga hoja yake juu ya msingi kwamba, Katiba inafaa kuwapo, lakini haipaswi kuwa jambo lenye uzito kiasi cha ‘kuteka’ mapokeo na nia chanya za viongozi waasisi katika nchi za Afrika, hususani kuhusu umoja wa nchi hizo na kupunguza wingi wa serikali zenye mamlaka kamili.
Ndiyo maana, Mkono anasema mfumo wa serikali tatu katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, utakuwa muendelezo wa mbinu za kikoloni, wenye lengo la kuwagawa wananchi na kutoa fursa pana ya uporaji wa rasilimali za nchi.
Hivyo anasema, kiongozi yeyote anayeutetea mfumo huo, hapaswi kuutumikia umma wa Tanzania, hasa katika nafasi ya Urais.
Kwa mujibu wa Mkono, Katiba si kitu kinachohitaji nguvu kubwa, badala yake nchi inaweza kuweka mambo ya msingi yan
ayopaswa kukubalikuwa, kufuatwa na kutekelezwa kama ilivyo kwa Uingereza.
“Wanaotaka serikali tatu, binafsi ninawaona kama wenye fikra mgando, hawayaishi mambo mema yaliyoasisiwa na viongozi katika nadharia ya kuwapo Afrika moja, tukagawanywa na wakoloni na sasa wanataka kuigawa Tanzania,” anasema.
Mkono anasema tangu wakati wa ukoloni, Waafrika walikuwa wamoja, wakitendewa uovu na wakoloni walioingia barani humo kwa lengo la kupora rasilimali zao.
“Sasa wanaotaka Tanzania igawanyike na kuwa na serikali tatu, wanafanya hivyo kutoa mianya ya wazungu kuendelea kupora rasilimali zetu, watu wa aina hiyo hawafai kuwa marais wa nchi hii,” alisema.
Mkono anasema hoja hiyo alitaka kuiwasilisha bungeni mjini Dodoma, lakini ikadhibitiwa kwa mujibu wa kanuni zinazotoa muda mfupi kwa Mbunge kuzungumza.
Hata hivyo, Mkono, anasema ili Tanzania ijiimarishe kwa umoja, amani, utulivu, maendeleo na ustawi wa jamii, inahitaji kubaki katika mfumo wa serikali moja na kuwa na kiongozi mkuu (Rais) anayesimamia maslahi ya umma pasipo mgawanyiko.
AWASHANGAA WARIOBA, SALIM
Mkono anasema, inashangaza kuona wajumbe wa Tume ya Marekebisho inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, kuwasilisha pendekezo la serikali tatu, huku wakiwa na uelewa wa kihistoria kuhusu umoja wa kuwapo umoja barani Afrika.
Ingawa hakuwataja kwa majina, Mkono, akaisema wapo watu waliowahi kuwa katika kundi G55 lililoibua hoja ya kuwapo serikali ya Tanganyika, na sasa wanataka kuifanikisha azma hiyo kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jaji Warioba, anatajwa kuwa miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walioibua hoja ya Utanganyika mwaka 1994, wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, ambayo hata hivyo, ilizimwa kwa msaada wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Mkono, anasema pia kuwa katika tume ya Warioba, yumo mjumbe aliyewahi kuwa kiongozi wa juu katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), aliyetekeleza jukumu ya kuihubiri ‘Afrika moja’, lakini sasa ameingia katika orodha ya wanaotaka kuigawa Tanzania.
Mjumbe wa tume hiyo, Dk. Salim Ahmed Salim, alikuwa Katibu Mkuu wa sita wa OAU, ambaye kumbukumbu zinaonyesha aliifanya kazi hiyo kati ya Septemba 19, 1989 hadi Septemba 17, 2001.

From: nipashe jpili

SUMAYE AWASHUKIA VIGOGO WA SERIKALI MADAWA YA KULEVYA

Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amewashukia ‘vigogo’ wenye madaraka, kuwa wanahusika kushamirisha biashara ya dawa za kulevya, wakiwatumia vijana katika kufikia malengo yao.
Sumaye amesema, mbali na ‘vigogo’ hao, biashara hiyo inawahusisha baadhi ya wafanyabiashara wenye nguvu kubwa za kiuchumi, na kusisitiza hakuna sababu kwa jamii kuogopa ama kulifumbia macho tatizo hilo.
Hata hivyo, Sumaye ambaye ni kiongozi pekee aliyehudumu wadhifa wa Uwaziri Mkuu kwa muda mrefu (miaka 10), hakuwataja kwa majina vigogo ama wafanyabiashara hao.
Lakini katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo taarifa zinazowahusisha baadhi ya wanasiasa, akiwamo Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) ambaye hata hivyo, alikana kuhusika katika biashara hiyo.
Pia, aliyewahi kuwa Mbunge kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), marehemu Amina Chifupa, aliwahi kutamka kuhusu kuwapo viongozi, wanasiasa na wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara hiyo, akitaka serikali iwashughulikie.
“Hili ni tatizo ambalo hatuwezi kulifumbia macho. Biashara ya dawa za kulevya inafanywa na watu wazito ama kwa fedha zao au kwa madaraka yao,” alisema Sumaye.
Sumaye alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa Kituo cha Maendeleo ya vijana (Tayodec) mjini Arusha jana.
Alisema hivi sasa nchi inaonekana kuwa kituo muhimu cha kupitishia dawa hizo kwenda ama kutoka katika mataifa mengine.
“Hii siyo sifa nzuri kwa nchi yetu. Lakini ukiachilia mbali madhara ya kupitishia nchini, dawa hizo zinawathiri sana vijana wetu na kuwageuza mazezeta kwa baadhi ya wale wanaozitumia,” alisema.
Kwa mujibu wa Sumaye, uhalifu mwingi wa kutisha unafanywa na watu wanaozitumia dawa hizo, huku vijana wanatumika kuzibeba kwenye miili yao, hali inayohatarisha maisha yao ikiwamo kufa.
“Cha kusikitisha wenye biashara hiyo wao hawaendi kuleta hizo dawa wala hawawatumii watoto wao, bali watoto wa wenzao ili wakikamatwa na vyombo vya dola au kudhurika kwa ubebaji huo, iwe ni shauri yao,” alisema.
“Hii ni roho mbaya tena ya kinyama sana, kuona wewe kupata fedha hizo chafu kwa gharama ya mtoto wa mtu mwingine, ati ni sawa tu. Lazima tujali watoto wa wenzetu kama watoto wetu,” aliongeza.

ASEMA ANAHUJUMIWA KWA VIJANA
Sumaye alisema Tayodec ni taasisi inayoshughulika na vijana, ikimteua kuwa mlezi wake, lakini akipata upinzani kutoka kwa watu wasiomtakia mema.
Alisema watu hao (hakuwataja majina), wameiona taasisi hiyo kama mtaji wa kisiasa na kutaka kuitumia kwa malengo hayo.
“Najua mmeshawishiwa kwa ahadi ya fedha nyingi na wakati huo huo kunikejeli mimi kuwa sina fedha. Nadhani hawakujua kuwa moja ya malengo makuu ya taasisi ni kupiga vita rushwa na tabia ya kununua watu na mngekubali kununuliwa basi ndiyo ungekuwa mwisho wa taasisi yenu,” alisema.

WAWILI WASIMAMISHWA JNIA
Wakati Sumaye akitoa angalizo hilo, maofisa wawili wa kitengo cha ukaguzi katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi unaohusishwa na kukamatwa kwa dawa za kulevya nchini Afrika Kusini.
Hivi karibuni, wasichana wawili wa Tanzania, Agnes Jerald (25) maarufu kama Masogange na Melisa Edward (24), walikamatwa nchini humo wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine, zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8, zikitokea hapa nchini.
Washitakiwa hao ambao walikatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo uliopo jijini Johannesburg, wakiwa na kilo 150 za dawa hizo zilizohifadhiwa kwenye masanduku sita.
Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Poul Rwegasha, aliimbia NIPASHE Jumapili kuwa kufuatia sakata la dawa hizo, wamewasimamisha kazi maofisa hao ambao hakuwataja majina wala taasisi wanazofanyia kazi, ili kupisha uchunguzi.
“Siku ya tukio hilo, tuliangalia kamera za usalama (CCTV) na kuwaona maofisa hao, hivyo tumewasimamisha kwa ajili ya uchunguzi na siyo kwamba wamefukuzwa kazi,” alisema.
Alisema kwa hatua hiyo, wameondolewa kwenye kitengo cha ukaguzi, ingawa bado wanafika kazini wakati uchunguzi dhidi yao ukiendelea.
Kwa mujibu wa Rwegasha, maofisa wawili wa polisi, ni miongoni mwa walioonekana kwenye CCTV hiyo, ingawa hakutaja majina yao.
Alisema hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuhusu kuhusika kwa askari hao, hivyo uchunguzi ukikamilika hatua zinazos
tahili zitachukuliwa.
“Siyo vizuri kukutajia majina ya hao maofisa kwani utaharibu uchunguzi wetu, na bado hawajakutwa na hatia, uchunguzi utakapokamilika nitakupatia taarifa,” alisema.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato, alisema zaidi ya watu 10 wamehojiwa kuhusiana na tukio hilo, na kwamba watajulikana pindi uchunguzi utakapokamili.

source: nipashe jumapili
 
Support : Copyright © 2013. Tanzania Mpya - All Rights Reserved
Template Modify by Hisia za Mwananchi
Proudly powered by Hisia